Makambo asepa zake kimyakimya

Muktasari:
- Makambo alijiunga na timu hiyo msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja unaoisha baada ya mechi ya mwisho kwa timu hiyo itakapocheza na Coastal Union keshokutwa Jumapili jijini Tanga.
KUNA taarifa zinaeleza mshambuliaji wa Tabora United, Heritier Makambo ametimka kambini, sababu ikitajwa ni kudai mshahara, hivyo akaona hakuja haja ya kuendelea kusalia katika timu hiyo.
Makambo alijiunga na timu hiyo msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja unaoisha baada ya mechi ya mwisho kwa timu hiyo itakapocheza na Coastal Union keshokutwa Jumapili jijini Tanga.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo ya Tabora ambayo juzi ilichakazwa kwa mabao 5-0 na Azam FC, kinasema kuwa, Makambo aliyewahi kutamba na Yanga na AC Horoya, FC Lupopo, DC Motema Pembe na Murooj ya Libya, ameondoka kimyakimya nchini.
“Makambo hajamuaga mtu yeyote, kaamua kuondoka kutokana na changamoto za kutokulipwa mshahara wake, jambo ambalo alitakiwa kukaa na kuzungumza na uongozi uone ni namna gani ya kutatua tatizo lake.,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, ofisa habari wa Tabora United, Christina Mwagala, alisema: “Mtu mzima hawezi kutoroka. Wachezaji wote wako kambini.”
Katika mechi alizocheza, Makambo ameonyesha kiwango cha kuisaidia timu, kutokana na uzoefu wake wa kucheza Ligi ya Tanzania na nje na amesifiwa kwa kuwa mhamasishaji wa wachezaji wenzake.
Straika huyo amehusika katika mabao 10 katika Ligi Kuu Bara msimu huu, akiifungia timu hiyo mabao sita na kutoa asisti nne, na kuiweka Tabora katika nafasi ya tano.
Makambo kwa mara ya kwanza kucheza Ligi ya Tanzania ilikuwa msimu 2018-19 akiwa na Yanga alipofunga mabao 17, kisha akaondoka kwenda Horoya ya Guinea kabla ya kurejea na kutua Tabora akiunda pacha kali na Yacouba Songne na Often Chikola.