West Brom waingilia dili la Samatta

Friday September 18 2020

 

By ELIYA SOLOMON

KWA mujibu wa mtandao wa The Sun, imeripotiwa kwamba  West Bromwich Albion F.C.  wapo kwenye mchakato wa kuipiga bao Fenerbahce kwenye kinyang'anyiro cha kuinasa saini ya mshambuliaji wa Aston Villa, Mbwana Samatta.

Miamba ya soka la Uturuki, walionekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili  nahodha huyo wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'  kwa mkopo huku kukiwa na kipengele cha kumalizana naye moja kwa moja mwishoni mwa msimu.

Inaelezwa kwamba Samatta ambaye aliichezea msimu uliopita Aston katika michezo 14 ya Ligi Kuu England na kufunga bao moja, anaweza kusepa kutokana na mpango uliopo ndani ya klabu hiyo.

Mapango wa Aston Villa kwa sasa ni kujaribu kuuza baadhi ya wachezaji wake kufuatia pesa nyingi zilizotumika kumnasa mshambuliaji wao mpya,Ollie Watkins ili kuwa na uwiano mzuri kati ya mapato yao na matumizi.

Kocha wa West Brom, Slaven Bilic anatajwa kuwa na mpango wa kukiimarisha kikosi chake ikiwemo idara ya ushambuliaji kufuatia kuanza kwao vibaya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England dhidi ya Leicester City, walipoteza kwa mabao 3-0.

Wakati akiwa Ubelgiji ambako alijipatia umaarufu mkubwa barani Ulaya akiichezea KRC Genk, Samatta aliifungia klabu hiyo mabao 76 kwenye michezo 191 katika uchezaji wake soka nchini humo.

Advertisement

Advertisement