Wenger asimulia bifu la Fergie

LONDON, ENGLAND. KOCHA, Arsene Wenger amekiri kwamba upinzani wake na Alex Ferguson na Jose Mourinho kuna nyakati ulizidi kipimo na kuwa vita kamili.

Kocha huyo wa zamani wa Arsenal, Wenger alihusika kwenye malumbano na mabifu na makocha tofauti kwa muda wake wa miaka 22 aliyokuwa akiinoa miamba hiyo ya Emirates.

Kocha wa Manchester United wa zama hizo, Fergie alikuwa mtu wa kwanza kuchukizwa na kuwasili kwa Wenger kwenye Ligi Kuu England mwaka 1996.

Wenger, ambaye aliondoka Arsenal mwaka 2018, alisema: “Upinzani kati yangu na Alex...

“Nilikuwa kocha wa kigeni niliyewasili kwenye Ligi Kuu England na kuja kutibua utawala wake, hivyo hakupenda.

“Alichukia kufungwa na nilichukia kufungwa, hivyo zilifika nyakati fulani mambo yalizidi na vita ikawa kali.

“Lakini, kwa kadri muda ulivyokuwa unasonga mbele, baada ya mchuano mkali, uhusiano wetu ukaanza kuimarika.

“Na hii leo kumekuwa na amani na ni marafiki.”

Hakukuwa na uhusiano mzuri pia baina ya Wenger na Mourinho, baada ya Mreno huyo kutua kuinoa Chelsea mwaka 2004.

Wawili hao wamekuwa na mechi nyingi za kiupinzani kwa miaka mingi sana na hata Mourinho aliporejea kuinoa tena Chelsea na baadaye kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Man United.

Mourinho aliwahi kumwambia Wenger ni ‘speshalisti wa kufeli’.

Wenger, 70, alisema: “Upinzani ule wakati mwingine ulikuwa binafsi sana na unakufanya ushindwe kujizuia. Unaingia kwenye mechi huku maneno mengi yamezungumzwa.”