Waziri Makamba: Serengeti Boys walipewa presha iliyowazidi umri

Wednesday April 24 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Siku chache baada ya Serengeti Boys kuondoshwa kwenye hatua ya makundi katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (Afcon U17), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Yusuph Makamba amesema timu hiyo ilipewa presha ya mashindano kulinganisha na umri wao.

Serengeti Boys ilifungwa mechi zake zote za Makundi dhidi ya Nigeria, Uganda na Angola katika fainali hizo zinazoendelea jijini Dar es Salaam na kukatisha ndoto ya kucheza kombe la dunia kwa vijana baadae mwaka huu Brazil.

"Bado tuna safari ndefu katika soka, tukumbuke tu hamasa ni hatua ya mwisho kwa mchezaji," alisema Waziri Makamba.

Alisema hata timu ya vijana ya Serengeti haikupaswa kupewa hamasa kubwa kama ambayo ilionekana wakati wa mashindano.

"Tuliwapa presha kubwa kulinganisha na umri wao, tuliwaaminisha kuwa Taifa wamelibeba wao, kitu ambacho kwa vijana wa umri wao hawakupaswa kupewa presha hiyo.

"Ambacho kingefanyika wangeambiwa tu kwamba wakacheze kama ambavyo wamekuwa wakicheza, lakini presha waliyopewa kwa ajili ya mafanikio kwenye mashindano ya Afcon iliwazidi umri," alisema.

Advertisement

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Advertisement