Wasso: Huyu Kaze, anzeni kushangilia

Saturday October 17 2020

 

By ELIYA SOLOMON

BEKI wa zamani wa kimataifa wa Simba na Yanga, Ramadhani Wasso, amewapa mzuka mashabiki wa Jangwani kwa kuwaambia waanze tu kushangilia sasa kwani Kocha Cedric Kaze aliyetua usiku wa juzi ni bonge la kocha na ataibeba sana kwani jamaa anajua sana kufundisha.

Wasso anayetoka nchi moja na Kaze yaani Burundi, alisema anachokisema sio kutaka kumpamba Kaze, ila ukweli Yanga imelamba dume kwa kocha huyo na anamfahamu jinsi anavyofundisha soka safi la kushambulia na kumiliki mpira.

“Ninamfahamu Kaze tangu 2012 ilikuwa kwenye mashindano ya Kagame akiwa na Atletico Olympic alitushangaza Yanga kwa kutufunga, aliisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, hatukuamini. Analijua soka la ukanda wetu,” alisema Wasso na kuongeza;

“Nakumbuka kikosi chake kilikuwa na Didier Kavumbangu kabla ya hajasaliwa na Yanga wakati huo alikuwa kwenye kiwango bora.”

Wasso alisema ni vema wachezaji wa Yanga sasa wakajiandaa kisaikolojia maana wakitaka kuingia kwenye mipango yake wanatakiwa kutumia zaidi akili kwenye uchezaji wao kuliko nguvu.

“Hakuna kitu kizuri kama mchezaji kujua aina ya kocha ambaye unaenda kukutana naye lakini nikiitazama Yanga ina wachezaji wenye uwezo wa kuendana na mpira wake,” alisema.

Advertisement

Wakati akitua nchini Kaze alisema amekuwa akifuatilia kila mchezo wa Yanga hivyo amewasoma wachezaji wake na ameandaa namna nzuri kwa wachezaji hao kuendana na mipango yake. Kaze pia amehusika kusajili wachezaji kadhaa wa kikosi hiki.

Advertisement