Wamekula umeme mechi za kwaza kwenye timu mpya

Muktasari:

Mara zote, wachezaji ambao wamekuwa wakianza vyema maisha mapya kwenye timu mpya wanaonekana watakwenda kuwa mashujaa, lakini wachezaji hao, mechi zao za kwanza kwenye timu mpya hazikuwa bora kwa upande wao na waliishia kuonyeshwa kadi nyekundu tu.

LONDON,ENGLAND.KILA mchezaji anaposajiliwa amekuwa na matamanio ya kuanza vyema katika timu yake mpya kwa sababu kutakuwa na watu wengi sana wanaotaka kumtazama atakavyofanya kwenye mchezo wake wa kwanza.

Mara zote, wachezaji ambao wamekuwa wakianza vyema maisha mapya kwenye timu mpya wanaonekana watakwenda kuwa mashujaa, lakini wachezaji hao, mechi zao za kwanza kwenye timu mpya hazikuwa bora kwa upande wao na waliishia kuonyeshwa kadi nyekundu tu.

7.Joao Miranda (Sochaux)

Joao Miranda atabaki kuwa mmoja kati ya mabeki bora wa kati katika kizazi chake, ambapo alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha Atletico Madrid kilichobeba ubingwa wa La Liga.

Lakini, mechi yake ya kwanza kucheza kwenye Bara la Ulaya baada ya kutoka kwao huko Brazil, ilikuwa na majanga huko Ligue 1 kipindi hicho akiwa katika kikosi cha Sochaux . Miranda aliishia kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika za mwisho. Hata hivyo, kikosi chake kilibadili matokeo ya kupigwa 1-0 na kushinda 2-1 katika mchezo huo.

6.Federico Fazio (Tottenham)

Beki Federico Fazio alinaswa na Tottenham Hotspur mwaka 2014 akitokea Sevilla kwa ada ya Euro 8 milioni. Lakini, mechi yake ya kwnaza huko Spurs haikuwa nzuri kabisa, aliishia kuonyeshwa kadi nyekundu alipowakabili Manchester City.

Beki huyo alijikuta kwenye majanga hayo baada ya kumchezea madhambi straika Sergio Aguero na kuleta majanga zaidi kwenye timu yake ikichapwa mabao 4-1. Baada ya hapo alicheza mechi 40 kwa zaidi ya misimu mitatu aliyokuwa kwenye timu hiyo kabla ya kutimkia huko AS Roma.

5.Walter Samuel (Real Madrid)

Kabla hajaikamata dunia na kufahamika kama moja wa mabeki bora kabisa duniani wakati huko akiwa Inter Milan, beki Walter Samuel alikuwa na kipindi kigumu kwenye kikosi cha Real Madrid kwa muda wa miezi 12 aliyodumu na timu hiyo. Kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 25, Walter Samuel alinaswa kwa ada ya Euro 25 milioni, lakini mechi yake ya kwanza haikuwa nzuri huko Bernabeu, wakati alipoonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya RCD Espanyol. Mechi hiyo ilimalizika kwa majanga zaidi baada ya Los Blancos kuambulia kipigo cha bao 1-0.

4.Laurent Koscielny (Arsenal)

Beki Laurent Koscielny amekuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri kwenye kikosi cha Arsenal katika miaka ya 2010, maisha yake ya mwanzo huko Emirates hatakuanza vyema kabisa. Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa mechi yake kwanza kwenye kikosi cha Arsenal ilikuwa chini ya Liverpool, tena kwenye uwanja mgumu wa Anfield. Katika mchezo huo, Koscielny alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika za mwisho kabisa baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano. Lakini, huo ulikuwa mwanzo tu, baadaye, Koscielny alicheza kwa kiwango kikubwa na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu huko Emirates.

3.Joe Cole (Liverpool)

Joe Cole alinaswa bure kutoka Chelsea, wakati kiungo huyo aliponaswa na Liverpool kipindi hicho ilipokuwa chini ya Kocha Kenny Dalglish. Kiungo huyo fundi mpira mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England kwenye kikosi hicho alicheza dhidi ya Arsenal na hakika mambo hayakuanza vyema kwa Mwingereza huyo huko Anfield, ambapo aliishia tu kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu beki Laurent Koscielny. Maisha ya Joe Cole huko Anfield hatakuwa matamu sana.

2.Gervinho (Arsenal)

Winga huyo wa Ivory Coast hakukuwa na mjadala kuhusu kipaji chake na ile kasi yake aliyokuwa nayo uwanjani ambayo iliwapa shida mabeki wa timu pinzani kumdhibiti. Ishu kubwa ya Gervinho ilikuwa ufiti wake, kwamba mechi moja alicheza vizuri sana, lakini nyingine ungeweza kumshangaa kama ni yeye. Licha ya kung’ara sana kwenye mechi ya kujiandaa na msimu mpya, mechi yake ya kwanza Gervinho huko Arsenal ambapo alicheza na Newcastle United haikwenda vizuri ambapo alionyeshwa kadi nyekundu na kujikuta akikumbana na adhabu ya kufungiwa mechi tatu zaidi.

1.Jonathan Woodgate (Real Madrid)

Beki, Jonathan Woodgate alinaswa na Real Madrid mwaka 2004, lakini kutokana na majeraha ya mara kwa mara, beki huyo alisuburi hadi Septemba 22, 2005 kucheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi hicho cha Los Blancos, ikiwa ni miezi 14 imepita tangu aliposajiliwa. Lakini, majanga yalianzia kwenye mechi yake ya kwanza tu, ambapo kwanza Woodgate alijifunga kabla ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kadi mbili za njano. Majeruhi yaliendelea kumwaandana Woodgate na kushindwa kufikia mafanikio.