Wakwenu wanayo?

JANA ilikuwa ni siku ya winga wa Simba, Bernard Morrison kuwakerakera mashabiki wa Yanga mitandao. Alitupia ndinga yake aliyonunuliwa na Bilionea Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’.

Morrison ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga anayependa kuwakejeli mashabiki wake mitandaoni, jana aliushukuru uongozi wa Simba kwa kumnunulia gari aina ya Nissan Fuga huku mchezaji mwenzie Luis Miquissone naye akikabidhiwa Crown Athlete. Luis alishazoea kuinjoyi Dar es Salaam na kibaskeli chake.

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo ni Luis na Morrison wamekabidhiwa magari hayo ikiwa ni moja ya makubaliano ndani ya mikataba yao ya kazi na gari ya Morrison thamani yake ni Sh14 milioni wakati gari la Luis ni Sh13 milioni.

Mmoja wa vigogo wa Simba ameliambia Mwanaspoti magari ya wachezaji hao wawili ambayo ni makubaliano kwenye mikataba yao yatabaki kuwa mali ya klabu.

Morrison aliweka gari hilo kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akiandika maneno na lugha ya Kiingereza ambayo yalikuwa na maana hii; “Ahsante bosi Mo Dewji, wewe ni kiongozi mkubwa, ahsante Simba, mnajua kutunza vizuri wachezaji wenu.”

Mwanaspoti pia limejiridhisha nyota mwingine Gerson Fraga raia wa Brazil nae amekabidhiwa Rav4 J.

Mbali na nyota hao, Simba ina mastaa wengi wanaomiliki magari yao huku wachezaji kadhaa wakiwa hawana magari kutokana na sababu zao binafsi akiwemo mkali wa mabao Meddie Kagere ambaye inadaiwa foleni za Dar zinamkera yeye ni Bajaji tu na gari za kukodi pakiwa na ulazima.

Wengine ambao hawana usafiri binafsi ni Larry Bwalya, Chris Mugalu, Ibrahim Ame, David Kameta ‘Duchu’ ambao wamesajiliwa msimu huu na kipa Ally Salim ambaye alipandishwa kutoka timu yao ya vijana.

Lakini funga kazi ya wanaomiliki magari makali zaidi Simba na thamani yake ipo juu ni Nahodha John Bocco na Jonas Mkude kila mmoja anatumia Harrier ambayo thamani yake kwa gari moja ni Sh25 milioni.

Wengine ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Ibrahim Ajibu,Erasto Nyoni na Gadiel Michael ambao kila mmoja anamiliki gari Crown Athlete na kila moja thamani yake haizidi Sh14 milioni.

Beki wa kulia Shomary Kapombe na Kennedy Juma wao kila mmoja anatumia Toyota Mark X ambayo thamani yake ni Sh12.5 milioni.

Kipa wao Aishi Manula, Hassan Dilunga, Said Ndemla, Miraji Athman, Mzamiru Yassin na Ch arles Ilanfya wao kila mmoja ana IST ambazo huuzwa kati ya Sh10.5 na 11 milioni.

Clatous Chama anatembelea BMW, Pascal Wawa Toyota Brevis lenye thamani ya kati ya Sh10 na 11 milioni.

Licha ya viongozi wa Simba kugoma kuzungumzia maisha hayo ya kifahari ya wachezaji wao kwa madai ni makubaliano binafsi Mwanaspoti limebaini kuna baadhi ya wachezaji wazawa ambao wametumia fedha za kununulia magari kufanya uwekezaji kwa ajili ya maisha ya badae.

Katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya wachezaji hususani wa klabu za Ligi Kuu wamekuwa wakiringiana magari makali, ingawa safari inaonyesha klabu nyingine hususani Yanga na Azam bado wachezaji wao wengi hawajapewa magari na wajipange kwa vile ndio kwanza msimu umeanza.