Unakijua kile kipigo cha mbwa koko ? hiki hapa

Wednesday June 12 2019

 

By Salim Said Salim

KILA ninapozitafakari rekodi za dunia za michezo mbalimbali zipo ambazo hunishangaza na kukataa kuziamini.

Lakini hatimaye baada ya kuhakikisha ni za kweli hujiliwaza kwa kujiambia mtu haifai kufanyia mchezo mambo ya michezo.

Baadhi ya rekodi unaposimuliwa habari zake unabaki kutabasamu na ukijiuliza ilikuwaje? Jawabu linalofuata ni kicheko. Miongoni mwa rekodi ambazo sidhani zitatokea kuvunjwa ni za mchezo wa mpira wa magongo katika uwanja wa barafu kwa wanawake.

Katika mashindano ya Bara la Asia na Oceania yaliyofanyika Latvia 1998 kikosi cha wanawake wa Korea ya Kusini waliwachapa wenzao wa Thailand 92-0 katika mchezo wa vijana wa chini ya miaka 18.

Wachezaji na viongozi wa kikosi cha Thailand waliporudi nyumbani kila mmoja alipewa zawadi ya nyanya 92 zilizowekwa vizuri katika paketi iliyoandikwa ‘Ahsante’.

Shirikikisho la Kimataifa la Mpira wa Magongo katika Barafu limesema hii ni rekodi ya dunia ya magoli mengi katika mchezo huu kwa kinamama.Rekodi nyengine ni ya wanawake wa Slovakia kuwafunga wenzao wa Bulgaria 82-0 (narudia 82-0) katika pambano la kutafuta tiketi ya kucheza fainali za michezo ya Olimpiki.

Advertisement

Slovakia walisukuma mikwaju 130 golini na kufanikiwa kupata idadi hiyo ya magoli ambayo ni ya wastani wa bao moja baada ya kila sekunde 44.

Bulgaria walihemewa kama vile walifungwa pingu za miguu na kutoweza kabisa kuwazuwia wapinzani wao waliowatawala kwa mbio, mbinu na ustadi.

Bulgaria iliongoza kwa 7-0 dakika 5 baada ya mchezo kuanza, 19-0 baada ya dakika 10 na 31-0 kilipomalizika kipindi cha kwanza.

Kikosi cha Bulgaria pia kilifungwa 30-1 na Croatia na 41-0 na Italia katika michezo mengine ya kundi hilo. Lakini vioja vya aina hii pia ni maarufu katika soka.

Kwa mfano Abroath iliifunga Bon Accord 36-0 baada ya kuongoza 15-0 wakati wa mapumziko katika Ligi ya Kuu ya Scotland 1885.

Kule Madagascar yalifanyika mambo siyo ya kawaida Oktoba 31, 2002 na tangu wakati huo siku hiyo hukumbukwa kwa tamasha linalohimiza mchezo safi na usio na uhuni.

Hii ilitokana na burudani usiyoweza kuilinganisha na yoyote ile ya mchezo huu duniani ya klabu zenye utani wa jadi na uhasama katika nchi hiyo AS Adema na SO I’Emyrne, zote za jiji la Antananarivo, vilipokutana kwa mchezo wa mwisho uliokuwa uamue ipi itakuwa klabu bingwa ya nchi hio.

Mchezo huu uliokuwa na vioja ulimalizika kwa Adema kuibuka na ushndi wa 149-0 na ambayo ndiyo idadi kubwa ya mabao kufungwa katika mchezo wa kandanda duniani.

Timu hizi miaka michache iliyopita zilikubaliana kukutana kwa mchezo wa kirafiki kuikumbuka siku ile iliyozusha kichekesho na hasira miongoni mwa vingozi na mashabiki wa kandanda.

Kilichotokea ni timu hizi mbili mara baada ya kuingia uwanjani, vingozi na wachezaji wa Emyrme kumkataa muamuzi Benjamina Razafintsalama.

Ombi lao lilikataliwa na shirikisho la kandanda la nchi hiyo na baada ya uamuzi huo Emyrne waliamua kuonyesha mchezo usio wa kawaida uliwaoudhi watazamaji wengi na kufurahisha watoto.

Watoto walipokuwa wakifurahia burudani hiyo mashabiki walivunja viti, milango na vifaa vya uwanja huku wakidai kurejeshewe fedha zao.

Hii ni kwa sababu walitarajia mchuano mkali ambao ulikuwa uamue timu ipi iwe bingwa na ipi ishike nafasi ya pili. Lakini tangu filimbi ya kuanza mchezo ilipopulizwa wachezaji wa Emyrne walisimama kama nguzo, hawakuhangaika na waliwaachia wapinzani wafunge magoli kwa raha zao.

Wapinzani wao walipokawia kufunga bao baadhi ya wachezaji wa Emryne waliukimbilia mpira na kwenda kujifunga wenyewe.

Wachezaji wawili walibaki kwenye goli wakati wote kuhakikisha wapinzani wao hawapuliziwi filimbi ya kuotea walipokwenda kufunga goli.

Kila walipofungwa goli waliruka na kupiga makofi kushangilia kama vile wao walifunga na wangechukua ubingwa.

Mpira ulipowafikia miguuni waliwapa pasi haraka wapinzani na kuwahimiza waende kufunga goli na golikipa siyo tu hakujaribu hata mara moja kuuzuwia mpira usingiie golini bali wakati mwingine aliharakisha kuusindikiza wavuni na haraka kuupeleka kati ili waendelee kufungwa magoli zaidi.

Shirikisho la Kandanda la Madagascar lilimfungia kocha, Zaka Be kwa miaka mitatu na mwenyewe kuomba adhabu yake iongezwe sufuri mbele ili isomeke 30 na wachezaji wanne wakafungiwa kwa msimu mmoja.

Tokea siku ile ikitokea timu Madagasacar kumkataa muamuzi Shirikisho la Kandanda lilimbadilisha haraka kwa kuhofia kutokea mkasa uliofanywa na klabu ya Emyrne.

Katika tamasha hili hutolewa fulana na beji zilizoandikwa 149-0. Wageni wanaoalikwa katika mchezo huo ni pamoja na wale waliofanya ule mkasa wa mwaka 2002.

Michezo mingine iliyokuwa na vituko ni ya ligi ya daraja la kati ya Nigeria iliyochezwa Julai 7, 2013 kati ya Plateau United

Founders dhidi ya Akurba FC na Police Machine FC dhidi ya Bubayaro FC.

Matokeo yalikuwa Plateau ilishinda 79-0 na Police ikaibuka kidedea kwa ushindi wa 67-0 na kuiwezesha Plateau United kupanda daraja kwa idadi kubwa ya magoli ya kufunga.

Katika michezo yote hii miwili zaidi ya nusu ya magoli wachezaji walijifunga wenyewe.

Aprili 11, 2001 Australia na American Samoa zilipambana katika mchezo wa kutafuta tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2002.

Australia iliweka rekodi ya kufunga mabao mengi katika mchezo wa kimataifa kwa kushinda mchezo huo baada ya kuifunga timu dhaifu ya American Samoa kwa magoli 31-0 na kusababisha FIFA kuanzisha hatua ya awali ya kufuzu kwa Kanda ya Oceania ili kuziepusha timu dhaifu kukutana na timu zilizozizidi mno ubora.

Kwa ujumla mchezo wa kandanda huwa na vituo ambavyo huvitegemei. Suala linalouulizwa ni kituko gani kipya kitaonekana siku za mbele.

Advertisement