Unai wa Arsenal, Ole wa Manchester United wameanza kuchonga

Muktasari:

Man United kwa upande wake imewekeza kwenye beki ili kuwa bora zaidi na hilo limejionyesha baada ya kushinda 4-0 kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya Chelsea.

London, England.Arsenal na Manchester United zote zimeanza vizuri kwa kushinda mechi zao za kwanza kwenye Ligi Kuu England.

Kocha Unai Emery na chama lake la Arsenal ameibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Newcastle United, shukrani kwa bao la straika Pierre-Emerick Aubameyang. Man United nayo chini ya Kocha Ole Gunnar Solskjaer, yenyewe iliichapa Chelsea 4-0, Marcus Rashford akifunga mara mbili, Anthony Martial na Daniel James wakipachika mabao mengine.

Vigogo hao msimu huu watachuana vikali kuhakikisha wanapata nafasi ndani ya Top Four ili kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita, ambapo Arsenal ilimaliza kwenye nafasi ya tano na Man United nafasi ya sita.

Katika kuweka mambo sawa, Arsenal imeonekana kuwekeza zaidi kwenye fowadi yake, ambao kwa sasa fowadi hiyo itakayoundwa na wakali kama Mesut Ozil, Aubameyang, Nicolas Pepe na Alexandre Lacazette imegharimu kiasi cha Pauni 217 milioni.

Man United kwa upande wake imewekeza kwenye beki ili kuwa bora zaidi na hilo limejionyesha baada ya kushinda 4-0 kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya Chelsea.

Usajili wa beki wa kati Harry Maguire umeifanya Man United chini ya Ole, ukuta wake ulioanza kwenye dhidi ya Chelsea kuwa na thamani ya Pauni 190.7 milioni. Katika mechi hiyo, Man United ilianza na mabeki, Luke Shaw, Victor Lindelof, Maguire na Aaron Wan-Bissaka.

Jambo hilo linaonyesha Man United na Arsenal zilivyopishana, ambapo Kocha Emery ameamua kuwekeza zaidi kwenye safu ya ushambuliaji, wakati Solskjaer ameamua kuwekeza kwenye safu ya ulinzi.

Fowadi yake, Arsenal ilimsajili Ozil kwa Pauni 42.5 milioni, Aubameyang Pauni 56 milioni, Pepe Pauni 72 milioni na Lacazette Pauni 46.5 milioni, huku Man United beki yake iliyoanza nayo dhidi ya Chelsea ikiigharimu, Shaw Pauni 30 milioni, Lindelof Pauni 30.7 milioni, Wan-Bissaka Pauni 50 milioni na Maguire Pauni 89 milioni.

Bila shaka, Emery fowadi hiyo iliyomgharimu Pauni 217 milioni, panga pangua ndiyo atakayotumia kwenye Ligi Kuu England msimu huu kuhakikisha kikosi chake kinamaliza ndani ya Top Four, sawa na ilivyo kwa Kocha Ole, ambaye haonekani kama atakuwa na chaguo tofauti kwenye safu yake ya ulinzi baada ya kuvutiwa na viwango vya mabeki wake hao kwenye mechi ngumu dhidi ya Chelsea.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa sasa, Man United inashika nafasi ya pili, ikizidiwa bao moja na Manchester City, lakini Arsenal nayo ikiwa na pointi sawa na wababe hao na tofauti iliyopo ni yenyewe ina bao moja tu la kufunga.

Mchezo ujao wa ligi, ndio utakaotoa taswira rasmi ya safu hizo mbili, ambapo Kocha Emery bila ya shaka ataanzisha wakali wake wote kwenye fowadi atakapokipiga dhidi ya Burnley uwanjani Emirates, wakati Solskjaer atakwenda kuipima beki yake kama ipo imara au ilikuwa zali tu Jumapili iliyopita wakati atakapoikabili Wolves ugenini uwanjani Molineux.

Shughuli pevu itakuwa wakati safu hizo zitakapomenyana zenyewe kwenye Ligi Kuu England, Septemba 28, ambapo kipute hicho kitapigwa Old Trafford.