UCHAMBUZI: Nguvu ya kikosi kipana Simba imeanza kupotea

TANGU msimu huu wa Ligi Kuu Bara uanze, Simba imepoteza mechi mbili ambapo imekusanya pointi 13 ikiwa imecheza mechi saba.

Simba ilipoteza mechi dhidi ya Prisons kwa bao 1-0 na mechi iliyofuata dhidi ya Ruvu Shooting bao 1-0, huku ikishinda michezo minne ikitoka sare mmoja.

Inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikitanguliwa na Azam wenye pointi 21, Yanga pointi 19 na Biashara United pointi 16.

Simba wanajiandaa kucheza na Mwadui FC ya mjini Shinyanga ambapo watakuwa nyumbani uwanja wa Uhuru huku wakihitaji kushinda ili kurejesha imani kwa mashabiki wao ambao sasa wanaonekana kuanza kukata tamaa na matokeo ya mechi mbili mfululizo.

Mashabiki wanalalamika kiwango cha timu yao lakini wanasahau kwamba mpira ndivyo ulivyo hata ligi zilizoendelea mabingwa huwa wanapoteza mechi ila wanavumilia na kutafuta njia mbadala kwa ajili ya mechi ijayo.

Tatizo ambalo linaonekana ndani ya Simba ni kwamba wasipocheza baadhi ya nyota waliozoeleka midomoni na machoni mwa mashabiki na wanapopata matokeo mabaya basi inakuwa ni shida ndani ya timu.

Shida kubwa na lawama anatupiwa kocha wao Sven pasipo kuangalia viwango vya wachezaji wao namna wanavyocheza kwa wakati huo ambapo baadhi yao wanaonekana kutokuwa na morali ya mchezo.

Hapo inapaswa kutafuta sababu kwanza ya kwanini wachezaji ama mchezaji fulani amecheza chini ya kiwango ndipo waje na suluhisho baada ya kubaini tatizo liko wapi.

Simba ndiyo timu inayosemekana ina kikosi kipana lakini hivi sasa inaanza kuonekana kile kikosi kipana hakina nguvu tena, hakina makali ya kubadilisha matokeo lakini ni nini chanzo cha wao kushindwa kubadilisha matokeo kwa wale wanaopata nafasi ya kucheza.

Ukiona hivyo ni wazi kuna shida na mojawapo ni mchezaji pengine hajapata nafasi ya kucheza mechi nyingi hivyo ule ufiti wa mechi unapungua na kupelekea kucheza chini ya kiwango.

Binafsi naamini kwamba Simba sio Meddie Kagere, Chris Mugalu, Clatous Chama ama John Bocco pekee ambao wanaaminika kuwa ndiyo bora zaidi kwa kuipa Simba matokeo mazuri.

Wengine wanasahau kuwa Simba ina nyota kibao ambao wanakaa nje kwa muda mrefu na wengine ambao walikuwa kikosi cha kwanza kama Erasto Nyoni ambaye huenda kuna sababu za hivi karibuni kutomiwa sana kikosini.

Kuna wachezaji wengine wazuri kama Gadiel Michael ambaye ameshindwa kufurukuta mbele ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Ibrahim Ajibu, Miraji Athuman ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao saba.

Wapo wengi tu wenye uwezo ndani ya Simba, lakini tayari kuna wachezaji wameaminika ambapo sasa wasipokuwepo kikosini inakuwa tabu, na tabu ninayoiona ni kwamba baadhi yao wamekata tamaa kwa kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Hata hivyo ikumbukwe kwamba maamuzi ya nani acheze anayo kocha ingawa kocha pia anatakiwa kuangalia ni namna gani atalinda viwango vya wale ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Ili nguvu ya kikosi kipana cha Simba tuendelee kuiona, basi kuna haja ya benchi la ufundi la timu hiyo kukaa chini na kutafakari namna gani watarudisha ile heshima ambayo ilikuwa inaonekana mwanzo ambapo hata kikiingia kikosi cha pili, basi mpira unapigwa haswa na matokeo yanakuwa mazuri.

Simba hawajachelewa kurudi kwenye mstari ila ile dhana ya kwanza mchezaji fulani ndiye anayeweza kuibeba timu iondolewe kwani matokeo mazuri ya timu hayapatikani kwa mchezaji mmoja pekee.

Pia hata wale wanaopewa nafasi ya kucheza baada ya wale wanaotumainiwa kukosekana basi waonyeshe kupambana ili kudhihirisha kuwa kukaa nje kwao si kwamba hawana uwezo.