UCHAMBUZI: Daraja la Kwanza sio kugumu, ngoma ipo VPL

Shirikisho la Soka nchini (TFF) ndiyo lenye mamlaka ya kusimamia ligi zote za soka nchini ingawa kuna Bodi ya Ligi (TPLB) ambao husimamia baadhi ya ligi ambazo ni Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL).

Ligi zingine zilizobaki husimamiwa na TFF yenyewe ukiachana na chombo hicho kilicho chini ya TFF.

Huo ni mgawanyo tu wa kupunguza majukumu ya shirikisho ambalo lina majukumu mengi.

Timu mpaka zishiriki ligi kuu zinakuwa zimepitoa ligi nyingi za huku chini hivyo ni safari ya miaka mingi ambayo inahitaji moyo wa kutokata tamaa.

Lakini kwenye shughuli ya kujua kipimo cha kupanda ligi kuu ni pale ambapo timu zinafikia hatua ya kucheza SDL na FDL ambayo hii ni hatua ya mwisho ya kupanda ligi kuu.

Hivi sasa mpaka kufikia msimu ujao wa ligi kuu timu nne zitashuka tena kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo sasa kwenye ligi zimebaki timu 18, msimu ujao zinatakiwa kubaki 16.

Hivyo kuna zitakazoshuka na zitakazopanda kutoka FDL.

Msimu huu timu mbili zimepanda kutoka FDL moja kwa moja ambazo ni Gwambina na Dodoma Jiji huku Ihefu yenyewe ikipenya kupitia mechi za mchujo.

Imeshuhudiwa namna timu hizo zilivyopanda daraja na zilivyokuwa zikicheza wakati zipo FDL na jinsi zinavyocheza baada ya kupanda daraja.

Zimeanza kwa kusota ingawa Ihefu ndiyo imesota zaidi katika mechi tano ambazo timu zote zimecheza.

Kama ingekuwa ligi inaelekea ukingoni basi wangekuwa kwenye hatari ya kurudi walikotoka.

Inasemekana FDL ni ligi ngumu lakini binafsi sioni kama FDL ni ligi ngumu labda ugumu ni pale inapofikia hatua ya mwisho ya kutaka kujua nani anapanda daraja ambapo kila mmoja ndiyo anaanza kutupia jicho.

FDL na SDL na ligi zingine za huku chini sidhani kama zina ugumu wowote, naamini hilo kwa sababu hatua za mwanzo hakuna anayefuatilia hata kama kuna madudu yanafanyika hayaonekani tofauti na ligi kuu ambayo ndiyo ligi ninayoona ina ugumu.

Ndiyo maana pia timu nyingi zinazopanda daraja zinaanza vibaya kwenye ligi kw asababu huku kila kitu kipo wazi.

Huku makandokando yote yanayofanywa yanaonekana wazi na watu wanayapigia kelele lakini huko chini hakuna anayepiga kelele wala kuyaona yanayotokea.

Ni ligi ambazo hazionyeshwi kwenye televisheni na hata zile timu zinaonyesha kuwa na upinzani utamu wake unaanza kufuatiliwa mwishoni napo kama zinafikia hatua nzuri ama kuonyesha dalili ya kupanda daraja na si vinginevyo.

Ligi hizo hazionekani popote ‘live’ labda usikie malalamiko baada ya mechi lakini kikubwa ambacho timu zinazopanda daraja zinapaswa kufanya ni kusajili wachezaji wenye ushindani na viwango vya juu ili kuendana na ligi ilivyo.

Timu zimeanza kutimua makocha, ilianza Yanga imefuata Ihefu kwa kumtimua Maka Mwalwisi aliyeipandisha daraja.

Ukiachama na Yanga usajili walioufanya unaonekana ni miongoni mwa sajili bora na kilichomuondoa kocha sio ubora wa kikosi inasemekana ni sababu nyingine.

Mwalwisi ametimuliwa kutokana na matokeo mabovu.

Ikumbukwe kwamba kocha huyo hata kabla ligi haijaanza uongozi ulikuwa haumuhitaji tayari walikuwa na mipango mingine ya kusaka kocha mpya lakini ilishindikana baada ya kuwepo kwa msuguano baina yao.

Mwalwisi ni kama alikuwa anasubiri muda tu wa kutimuliwa huenda hata kama amatokeo yangekuwa mazuri lakini huko mbele wangeachana naye maama nia yao ni kuwa na kocha mwingine na si huyo.

Lakini bado uongozi wa Ihefu unapaswa kuangalia pia namna ya usajili wao walioufanya na mahitaji ya ligi kuu maana huku sio FDL kuwa hawataona uwezo wa wachezaji wao huku kila kitu kipo wazi mwanzo mwisho hivyo hata ubora wa kikosi chao utaonekana zaidi.

Nina mashaka hata kocha atakayeingia kama atapata matokea mazuri zaidi kwa namna usajili wao ulivyo, inawezekana ama isiwezakane na pengine wakarudi kucheza FDL kama hawatakuwa makini kuboresha kikosi wakato wa dirisha dogo ila kikosi chao kikibaki hivi hivi basi tutajionea mengi kwa Ihefu.

Hivyo basi ninachoamini ni kwamba FDL haina ugumu wowote maana wengi hawaoni yanayoendelea huko chini bali ngoma nzito ipo Ligi Kuu Bara ambayo haifichi kitu - kama timu imepanda daraja kwa bahati mbaya basi huku ndo kipimo chao kikubwa.