Tukutane mwakani

Tuesday May 14 2019

 

LONDON, ENGLAND.TUKUTANE mwakani, lakini huko pembeni Manchester City wanazidi kufuliza. Pengine hilo ndilo lililobaki kwa makocha Jurgen Klopp na Pep Guardiola kutambiana kwenye Ligi Kuu England baada ya vita yao ya msimu huu kumalizika kibabe.

Makocha hao walikwenda jino kwa jino katika mbio za ubingwa baada ya vikosi vyao kutofautiana pointi moja tu, Manchester City wakibeba kwa pointi 98 dhidi ya 97 zilizovunwa na Liverpool baada ya mechi 38 katika ligi hiyo. Kocha Klopp amegomewa kumaliza ukame wa miaka 29 ya kusubiri taji hilo la Ligi Kuu England, lakini akimini kwamba huu ni mwanzo mzuri wa kile watakachokwenda kufanya msimu ujao.

Klopp alisema: “Man City wamekuwa na kiwango bora, lakini nasi tulikuwa bora. Tutakwenda kupambana tena, tunaamini tutafanikiwa kwenye hilo.

“Najivunia sana timu hii, timu spesho na najivunia kuwa sehemu ya hii timu. Kwa sasa tuna fainali kubwa inakuja, tunapaswa kujivunia. Yote tunawapongeza Man City, lakini tukatane kwa mapambano mwakani.”

Kocha Guardiola, ambaye amekuwa kocha wa kwanza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England ndani ya miaka 10 iliyopita, alisema: “Tunawapongeza Liverpool na tunawashukuru sana kwa sababu wametupa hamasa ya kupambana na kufikia viwango vyetu kutoka pale tulipoishia msimu uliopita.

“Kwa sababu tumepambana dhidi yao, ndio maana tumefanya vizuri. Jambo zuri kuvuna pointi 198 katika misimu miwili. Kushinda mara mbili mfululizo hilo ni jambo bora kwetu.”

Advertisement

Makocha hao kila mmoja bila shaka ataingia sokoni kwenye dirisha lijalo la usajili kuboresha kikosi chake tayari kwa mapambano ya msimu ujao Liverpool wataingia uwanjani kwa hasira kutaka kubeba taji hilo, huku Guardiola akisaka rekodi ya kubeba taji lake la tatu mfululizo.

Advertisement