Tengeru, Tanesco zapaa 16 Bora

Muktasari:

Kocha wa Tanesco, Fidelis Almas alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatinga robo fainali ambapo kwa sasa anakiweka sawa kikosi chake kwani anajua hatua hiyo ni ngumu hivyo lazima wajipange.

MASHINDANO ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (Shimmuta) imeendelea kushika kasi baada ya Chuo cha Tengeru na Tanesco kuwa timu za kwanza kutinga 16 bora upande wa soka.

Michuano hiyo inashirikisha timu za mashirika na taasisi 46 katika michezo ya soka, kikapu, kuvuta kamba, netiboli, mpira wa mikono, riadha na mchezo wa bao.

Tanesco wametinga 16 Bora baada ya kufikisha pointi tisa kundi B huku Tengeru wakiwa washindi wa pili kwa alama sita na kufanya timu hizo mbili kuwa za kwanza kutinga hatua hiyo.

Kocha wa Tanesco, Fidelis Almas alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatinga robo fainali ambapo kwa sasa anakiweka sawa kikosi chake kwani anajua hatua hiyo ni ngumu hivyo lazima wajipange.

Alisema msimu huu wamejipanga ipasavyo kutwaa ubingwa huo kwani amefanya maandalizi ya nguvu hivyo ana wasiwasi katika mashindano hayo kwani wachezaji wake wapo fiti.

“Tumefikia hatua ngumu sana hivyo ninakiandaa kikosi changu ili nikiweke fiti. Kikubwa kwa sasa naboresha tu safu ya ulinzi na ushambuliaji ambazo zimefanya vizuri katika hatua ya makundi,” alisema kocha Almas.

Katika mchezo mwingine wa mpira wa wavu, Chuo Kikuu cha Teknolojia Mbeya (Must) kiliwafunga Sua kwa seti 2-0 huku Chuo Kikuu cha Mzumbe wakiwafanyia mbaya TBS kwa kuwatandika seti 2-0 katika michezo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mirombo jijini hapa.