Tanzanite Queens yatua

Tanzanite Queens wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere baada ya kutwaa ubingwa wa vijana chini ya umri wa miaka 20 yanayoandaliwa na COSAFA

Muktasari:

  • Tanzanite Queens imeshiriki Fainali za COSAFA kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 20 kama timu mwalikwa ikiwa ni mara yake ya kwanza.

Kundi kubwa la mashabiki na wadau wa soka wamejitokeza kuilaki timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 'Tanzanite Queens' iliyowasili leo usiku kutokea Afrika Kusini.

Timu hiyo imetoka kutwaa ubingwa wa mashindano ya wanawake wa umri huo yanayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA).

Tanzanite Queens imeshiriki mashindano hayo kama mgeni mwalikwa na jana ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Zambia kwa mabao 2-1 kwenye mechi ya fainali iliyochezwa jijini Pretoria.

Akizungumza baada ya kuongoza mapokezi ya timu hiyo, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza alisema kuwa timu hiyo imeitangaza vyema nchi na inatoa matumaini kwa siku za usoni.

"Timu hii imefanya kazi kubwa na nzuri kwanza kwa kupambana hadi ikaweza kutwaa ubingwa lakini pia mchezaji bora wa mashindano ametoka kwenye timu yetu.

Wameonyesha kuwa wanaweza na hii inamaanisha kwamba tukifanya uwekezaji mzuri kwa vijana na hasa wanawake tutafanya vizuri," alisema Waziri Shonza.

Mbali na Shonza, wengine waliokuwepo katika mapokezi ya timu hiyo ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Mkurugenzi wa Wizara ya Michezo, Yusuph Singo.

Pia kulikuwa na Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, katibu wake, Wilfred Kidao na mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya shirikisho hilo, Alhaj Ahmed Mgoyi