TACIP yazinduliwa rasmi jijini Dodoma

Muktasari:

Mradi huo unadhamira ya kuwajengea mazingira wezeshi wasanii wa sanaa za ufundi kutumia ujuzi na ubunifu wao kujikwamua na umasikini huku wakiongeza mchango katika pato la taifa

Dar es Salaam. Mradi wa utambuzi wa wasanii wa Sanaa za ufundi Tanzania ujulikanao kama (TACIP) umezinduliwa rasmi Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Adrian Nyangamalle pamoja na Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Godfrey Mungereza jijini Dodoma leo.

Akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, Mwenyekiti wa Bunge la Tanzania, Najma Giga alisema wameupokea mradi wa Tacip kwa faraja kubwa katika jiji lao na makao makuu ya nchi, jambo jema kwamba mradi huu uliobuniwa na kampuni  ya (DataVision International 'DVI').

DVI ikishirikiana na Shirikisho la Sanaa za ufundi nchini chini ya wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo kupitia BASATA unadhamira ya kuwajengea mazingira wezeshi wasanii wa sanaa za ufundi kutumia ujuzi na ubunifu wao kujikwamua na umasikini huku wakiongeza mchango katika pato la taifa.

“Natoa wito kwa serikali ya Dodoma kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa kusaidia katika kutoa wito kwa jamii na hata katika kutatua changamoto watakazo kutana nazo pindi wakifanya shunghuli zao jijini hapo,” alisema Giga.

Naye Mratibu wa TACIP, Sauli Mpocke alielezea hadhma ya mradi wa TACIP katika  kuwafikia wasanii wote nchini wa tasnia ya sanaa za ufundi kwa lengo kuu la kupata taarifa za wasanii kwa kuwabaini na kuwatambua ili kuwaunganisha katika fursa mbalimbali na kusaidia kutatua changamoto zinazo wakabili.

“Kazi ya kutambua na kuwasajili wasanii lilianza rasmi jijini Dar es salaam, ambapo tumetembelea na tunaendelea kutembelea wilaya zote za jiji hilo,  na sasa tumeingia rasmi mkoani Dodoma tukiwa na dhamira ile ile ya kupita mtaa kwa mtaa kwa nia ya kutimiza lengo la kumfikia kila msanii kwenye wilaya zote na nchi nzima kwa ujumla,” alisema  Mpocke.