Straika aingiza njeve kocha AFC Leopards

Tuesday March 10 2020
Pic mshambulaiji

Nairobi, Kenya. STRAIKA Elvis Rupia anayezidi kuonyesha kiwango Ligi Kuu ya KPL, sasa kamwingiza njeve kocha wake, Antony Modo Kimani pale klabuni AFC Leopards.

Tangu aliposajiliwa na Ingwe dirisha dogo la Januari kutoka Wazito FC, Rupia kawa kwenye fomu ya kutisha sana.

Juzi Jumapili kwenye Mashemeji Derby iliyopigwa kati yao na watani wao wa jadi ambao kwa sasa ni vinara wa ligi kuu Gor Mahia, Rupia aliendelea kuonyesha ubora wake.

Japo hakufanikiwa kufunga akipoteza fursa mbili za wazi, Rupia alionekana kuwapa mabeki wa upinzani wakati mgumu sana kutokana na janja zake pamoja na mikimbio aliyokuwa akifanya.

Ili kumzima, Gor waliamua kutumia wachezaji wawili kila alipopokea mpira.

Kiwango chake kizuri tangu Januari kimemwezesha kuipachikia Ingwe mabao matano kutokanana na mechi sita alizocheza mpaka sasa.

Advertisement

Kule Wazito alikuwa akitumika sana kutoka benchi ila bado alifanikiwa kuwafungia mabao manne. Hata hivyo uamuzi wa Kocha Kimani kumchukua ili kujaza pengo lake John Makwatta aliyewakimbia na kurejea zake Zambia, umeonekana kuzaa matunda kwani jamaa anajiamini zaidi na anapata muda mwingi wa mchezo.

Kuiva huko kwa Rupia aliyefikisha mabao tisa kwenye ligi kuu ndio sasa kunamtesa Kocha Modo. Jamaa kapaniki tayari.

Hii ni kwa sababu tayari klabu kadhaa zimeanza kumuulizia Rupia. Ubaya Rupia aliuzwa na Wazito kwa mkopo. Kibaya hata zaidi ni Ingwe wamesota kinoma hivyo Kocha Modo hana uhakika ikiwa klabu itakuwa na fedha zitakazowawezesha kumsajili Rupia kwa mkataba wa kudumu, pia kumpa mkataba mzuri.

“Rupia ni mchezaji mzuri sana, mchango anaouleta kwenye timu ni mkubwa sana. Ni aina ya mchezaji ambaye kocha yeyote angelipenda kuwa naye kwenye kikosi chake. Ila cha kusikitisha, sina uwezo wa kumzuia asiondoke. Uamuzi huo upo kati yake na klabu yake ya awali Wazito FC ila ingelikuwa ni uwezo wangu, ningelipenda kumwona akiichezea AFC Leopards msimu ujao,” Modo kasema.

Modo anasema kiwango cha Rupia kimezifanya klabu kadhaa nje na ndani ya nchi kumuuliza na hivyo kumfanya awe na hofu.

Advertisement