Stars, Burundi kuziweka kiporo Simba, Yanga Ligi Kuu

Wednesday September 30 2020

 

By Majuto Omary

Dar es Salaam. Mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga iliyopangwa kufanyika Oktoba 18 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ipo shakani kutokana na mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu yanayotarajiwa kufanyika wakati wowote.

Taarifa kutoka ndani ya Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB), zilisema jana kuwa chombo hicho cha kuendesha ligi za mpira wa miguu nchini kinalazimika kubadili ratiba hiyo kutokana na mechi ya kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (Fifa) kati ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na Burundi iliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Oktoba 11.

Awali, ratiba ya Ligi Kuu iliyotolewa na TPLB na Shirikisho la Soka nchini (TFF), haikuweka nafasi ya mchezo huo kuchezwa bila ya kuahirisha mechi za ligi na tayari TFF imekwishaeleza uwepo wa mechi hiyo.

Tayari TFF imetangaza kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije atatangaza majina ya wachezaji wa timu ya Taifa Oktoba 2 na baadaye wataanza kambi baada ya mechi za Ligi Kuu zilizopangwa kufanyika Oktoba 3, 4 na 5.

Kutokana na hali hiyo, mechi za Oktoba 9, 10, 11 zitaahirishwa ikiwamo ya Yanga na Simba kutokana majukumu ya Taifa Stars na kupangiwa siku nyingine.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Oktoba 9 kulikuwa na mechi kati ya Azam FC na Mwadui FC wakati Biashara United ilikuwa icheze na Ihefu SC.

Advertisement

Mechi zilizokuwa zichezwe Oktoba 10 ambazo pia zitaahirishwa ni JKT Tanzania dhidi ya Ruvu Shooting, Gwambina FC dhidi ya Mtibwa Sugar pamoja na ile ya Tanzania Prisons dhidi ya Simba iliyopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Timu za Yanga na Polisi Tanzania ambazo zilikuwa zicheze Oktoba 11 nazo hazitacheza kutokana na majukumu ya Taifa Stars. Mechi nyingine ambazo zilipangwa kuchezwa siku hiyo ni KMC dhidi ya Coastal Union na Dodoma Jiji dhidi ya Mbeya City.

Mabadiliko ya ratiba hayo pia yataikumba mechi ya Namungo FC dhidi ya Kagera Sugar iliyopangwa kufanyika Oktoba 12.

Akizungumzia suala la ratiba ya timu ya Taifa kucheza mechi ya kimataifa, ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo alikiri kuwa watabadili ratiba ya ligi kutokana na majukumu ya Taifa Stars.

Kasongo alisema ratiba ya awali haikutoa nafasi kwa ajili ya timu hiyo kutokana na sababu mbalimbali lakini sasa watalazimika kufanya mabadiliko ambayo hawawezi kuyaepuka.

“Siwezi kuzungumzia mabadiliko ya mechi ya Yanga na Simba, mimi nazungumzia mabadiliko ya ratiba nzima ambazo zimeingiliana na ratiba ya mechi na kambi ya timu ya Taifa,” alisema Kasongo.

Hatahivyo, alisema hawezi kuingia undani wa taarifa hizo akisisitiza wadau wa soka wasubiri kuona mabadiliko ya ratiba.

 

Advertisement