Stam: Alliance watapata tabu

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Stam alisema mchezo huo wanauchukulia kama fainali kwao kwani wakishinda watakuwa angalau kwenye nafasi nzuri ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

SIMIYU.KIKOSI Biashara United kinaingia uwanjani kikiwa na hasira kali chini ya kocha wao Amri Said ‘Stam’ ambao wanajipanga kuivaa Alliance.

Stam amesema patachimbika mjini Musoma pale Biashara United yenye ‘mzuka’ watakapowavaa Alliance FC katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Karume mjini humo mbele ya mashabiki wao wanaotaka kuona wanavuna alama tatu na sio kitu kingine ili kuzidi kukaa kukwepa mstari wa hatari kwenye Ligi Kuu.

Mtanange huo utakuwa kama vita ya kulipiza kisasi kwani katika mchezo wa mzunguko wa Kwanza Alliance walishinda mabao 2-0 katika mtanange uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Mpaka sasa Alliance wana pointi 41 wakiwa katika nafasi ya 13 huku Biashara wakiwa na alama 40 katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Stam alisema mchezo huo wanauchukulia kama fainali kwao kwani wakishinda watakuwa angalau kwenye nafasi nzuri ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Alisema kikosi chake kwa sasa kipo katika fomu nzuri jambo ambalo limempa nguvu ya kupambana na kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

“Kikosi changu kipo sawa kwa sasa nimepata nguvu kuona safu ya ulinzi na ushambuliaji imeimarika sana hivyo sina wasiwasi katika mapambano haya,” alisema Stam akisisitiza kutaka kulipiza kisasi.