Solskjaer awakingia kifua mabeki wake

MANCHESTER ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amewakingia kifua mabeki wake na kusisitiza kwamba safu hiyo ya ulinzi ni nzuri na anaamini itaimarika zaidi kila mechi.

Kocha huyo kwa sasa yupo kwenye presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Crystal Palace ndani ya Old Trafford kwa mabao 3-1.

Katika dirisha hili amefanikiwa kuipata saini ya kiungo kutoka Ajax, Donny van de Beek lakini swali limebaki kwenye safu ya ulinzi ambayo wanacheza Harry Maguire na Victor Lindelof ambao wanaonekana kufanya makosa mengi yanayoigharimu timu.

Ili kushinda 3-2 juzi, United walihitaji penalti waliyopewa ‘usiku’ huku ya firimbi ya kumaliza mechi ikiwa imeshapulizwa, shukrani kwa uamuzi wa VAR uliowarudisha wachezaji uwanjani. Baada ya kumalizika mchezo huo, Solskjaer alisema: “ Msimu uliopita walionyesha namna wanavyoweza kuzuia kwa ubora, ni kweli mechi iliyopita hatukucheza vizuri kwa kuwa tulifungwa mabao mengi, lakini takwimu zetu za msimu uliopita zinaonyesha ni jinsi gani tunaweza kuzuia kwa ubora,” alisema.

“Harry Magure na Eric Bailly walikuwa na muunganiko mzuri katika msimu uliopita, hivyo namsubiri Bailly awe sawa ili aje kucheza na Magure,” aliongeza Ole akisisitiza: “Najiamini sana.”