Siri ya wanasoka kujifua ufukweni hii hapa

Thursday May 14 2020

 

By Dk. Shita Samwel

Tangu fununu za kutaka kuanza kwa ligi mbalimbali duniani bila kuwapo kwa mashabiki, tayari hapa bongo wachezaji kadhaa wameonekana kujiongeza kimtindo na kuanza kujifua maeneo ya ufukweni.

Katika fukwe za Zanzibar nyota watatu wa Yanga ambao ni wenyeji wa Unguja, Adeyum Saleh, Abdulaziz Makame na Feisal Salimu ‘Fei Toto’ wanafanya mazoezi ya soka ya vikundi vidodogo ili kujiweka fiti.

Walifanya hivyo huku wakizingatia ushauri wa wataalam wa afya ili kujikinga na homa kali ya mapafu ya COVID-19 na huku wakifanya mazoezi ya kuwapa utimamu wa mwili na huku wakijijenga kimbinu.

Kwa upande wa bara katika fukwe za Dar es Salaam kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima alionekana akijifua mwishoni mwa wiki iliyopita katika ufukwe wa Escape One.

Nyota huyo wa nchini Rwanda alipanga vifaa vya mazoezi vinavyosaidia kumjenga kimbinu na kumpa utimamu wa mwili, alivitumia kwa mtindo wa kuviruka kama mruka viunzi na huku akukimbia kimbia mchangani.

Vile vile beki wa kati wa klabu ya Simba, Serge Pascal Wawa kutoka nchini Ivory Coast naye pia ameonekana akifanya mazoezi mchanganyiko ya binafsi ikiwamo ya kunyoosha na kuimarisha misuli na yale ya kimbinu.

Advertisement

Tofauti na kina Fei Toto waliobuni mtindo wa kucheza kwa kikundi kidogo wakieleza mtindo huwa unawapa ari wakati kina Niyonzima na Wawa walikuwa wanajifua wenyewe na wakati mwingine kujichanganya na wenzao kina Juma Kaseja na wengine bila ya kujali wanatoka klabu tofauti, Simba, Yanga, Azam na nyinginezo.

Kwa kuzingatia tahadhari zote ikiwamo kuvaa barakoa na kuwa na umbali wa mita angalau moja kati ya mchezaji na mchezaji mazoezi ya mchangani ni mazuri sana.

Siri kubwa ya ufanyaji wa mazoezi ya ufukweni kwa wanasoka ni kutokana na mazoezi hayo kuchoma zaidi kiasi kikubwa cha mafuta yaliyorundikana mwilini.

Wachezaji hao ambao wanashiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara wameamua kujifua kivyao kwa kutumia fursa za ufukweni ambako huwa na eneo kubwa, mchanga mwingi, hewa ya kutosha na utulivu mwingi.

Uchanganyaji wa mazoezi ya kukimbia ufukweni pamoja na kuogelea baharini yana faida kubwa kwa mchezaji kwani anapata utimamu bora wa mwili na hatimaye kulinda pia kiwango chake.

Ufanyaji wa mazoezi ufukweni ni moja ya mbinu ambayo inatumika sana kwa miaka mingi na wanasoka wengi wa Kibrazili na kuwa kama utamaduni kwa ajili kujiburudisha na kutengeneza utimamu wa mwili

Je unazijua faida za

mazoezi ya ufukweni?

Zoezi hili humfanya mchezaji kuchoma kiasi kikubwa cha sukari (mafuta) ya mwilini kwa vile wakati anakimbia au kucheza soka, misuli ya miguu hutumia nguvu nyingi kukimbia na kucheza.

Ufukweni kuna mchanga mwingi sana wakati wa kukimbia miguu huzama katika rundo la mchanga hivyo kuipunguza kasi na kuhitaji kutumia nguvu kuinyanyua tena ile kupiga hatua na kikimbia.

Hali hii ndiyo inayochangia mwili kutumia nguvu nyingi sana ili kuweza kucheza na kukimbia na hivyo kumfanya mchezaji kupunguza uzito na hatimaye kuwa mwepesi.

Vile vile mchezaji anapokuja katika uwanja wa kawaida huwa na wepesi na kuweza kujiamini na kutohisi kuchoka kutokana na mazoea ya mwili na akili kutumia nguvu katika mchanga wa ufukweni.

Faida ya pili ni kuimarisha na kujenga misuli ya miguu, mchezaji soka yeyote uimara wa miguu yake ndiyo kila kitu kwani ndiyo huitumia kucheza soka.

Zoezi la ufukweni huifanya misuli ya mwili ya miguuni kutumia kiasi kikubwa cha sukari ili kukunjuka na kuweza kuutembeza mwili wakati wa kukimbia na hatimaye huifanya kuwa mikakamavu na kujengeka.

Hali hii pia husaidia kuifanya misuli ya miguu kuwa imara na kuweza kuhimili majeraha yatakanayo na michezo huku pale inapopata huweza kupona haraka na kwa wakati.

Kutokana na kukaa sana bila mazoezi misuli na maungio huweza kuwa na uchovu hivyo kushindwa kuwajibika kwa ufanisi wakati wa kucheza. Unapofanya mazoezi haya husaidia kulainisha viungo na kuwa vyepesi.

Kutokana na upana wa eneo la ufukweni na kuwa wazi huku likisindikizwa na upepo mwanana uliosheheni hewa safi yenye oksijeni humfanya mchezaji anayefanya mazoezi kupata hewa ya kutosha.

Hii huwa na faida kwa moyo na mzunguko wa damu na mwili kuweza kupata hewa ya oksijeni kwa wingi.

Hali ya ufukweni huweza kumpa burudani mchezaji na kusahau mambo yanayompa msongo wa mawazo ikiwamo hofu ya yeye binafsi, ndugu, jamaa au wazazi kuugua corona.

Ufukwe ni eneo la burudani na hata wanasaikolojia wanashauri kwa mtu mwenye shinikizo la akili au msongo wa mawazo kwenda ufukweni kwani wanaamini mazingira hayo husaidia kupeperusha hasira, huzuni, msongo wa mawazo na shinikizo la akili.

Baadaye mwanasoka anapomaliza mazoezi ufukweni na kuamua kuogelea ndipo huzidi kupata utimamu na wepesi kwenye maeneo mengine ya mwili.

Hii ni kwasababu ya zoezi la kuogelea linashika namba moja kuimarisha kujenga maeneo mengi ya mwili kutokana na zoezi hili kuhusisha misuli mingi ya mwili.

Hivyo mchezaji hupata kasi na wepesi na misuli huwa imara na yenye nguvu anapochanganya mazoezi ya ufukweni na kuogelea.

Je unazijua hasara za

kucheza ufukweni?

Mchezaji anayecheza peku peku maeneo hayo anaweza kupata vijeraha vya nyayoni kutokana na uwepo wa vitu vyenye ncha kali ikiwamo nyumba za konokono au mazao mengine ya baharini na miba ya samaki na vitu kama chupa zilizotupwa kiholela.

Kutokana na kuwepo kwa mchanga mwingi unaozamisha eneo la chini la miguuni, mchezaji anaweza kupata majeraha ya kifundo cha mguu na magoti.

Kwakuwa mazoezi haya huupa ugumu mwingi sana mwili wakati wa kufanya pale atakapoyafanya kupita kiasi bila kujipa mapumziko anaweza kujipa uchovu na majeraha.

Upepo mkali unaweza kuwa chanzo kupata mafua ya muda na vile vile mchanga unaorushwa machoni unaweza kukereketa machoni.

Pamoja na hasara hizi chache lakini faida ya kujitenga na kufanya mazoezi ya ufukweni na kuogelea baharini ni kubwa zaidi kwa mwanasoka anayejitenga kujikinga na maambukizi ya corona.

Advertisement