Simba yatua Tanga matumaini kibao kuichakaza Coastal Union

Monday April 15 2019

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Kikosi cha Simba kimeondoka leo Dar es Salaam asubuhi kwenda Tanga tayari kwa mchezo wao dhidi ya wenyeji wao Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani.

Ikumbukwe ligi licha ya kuwa inaelekea ukingoni Simba ambao wametoka kuendolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika hawajacheza mchezo wowote na Coastal msimu huu na hiyo ndio inakuwa mechi ya kwanza kukutana kwao.

Licha ya kufungwa mabao 4-1, ugenini dhidi ya TP Mazembe na kutolewa katika hatua ya robo fainali wachezaji na benchi la ufundi wa timu ya Simba wamegeuka kuwa kivutio kwenye Hoteli ya Tanga Beach Resort.

Wachezaji hao mara baada ya kuteremka kwenye gari wakiwa wanaingia hotelini walisimamishwa kwa muda shughuli zao na kujipanga kuwaangalia na wengine walikuwa wakipiga nao picha.

Wachezaji hao wapo Tanga kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi yao na timu ya Coastal Union utakao fanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani Jumatano ya wiki hii.

Walipowasili kwenye hoteli hiyo moja kwa moja walikwenda kupata chakula cha mchana na kisha kuelekea kwenye vyumba vya hoteli hiyo kupumzika kabla ya jioni kwenda kufanya mazoezi.

Kocha mkuu Patrick Aussems alipoingia kwenye mlango wa kuingilia hotelini humo aliwasalimia watu waliosimama pembeni kwa kuwaambia "Habari zenu Mabibi na Mabwana," kisha akaeingia hotelini.

Advertisement