VIDEO: Waziri Ummy ataka ubingwa Coastal Union

COASTAL UNION YARUDI KIBABE LIGI KUU

Muktasari:

Misimu miwili iliyopita timu tatu za mkoa wa Tanga, Coastal Union, African Sport na Mgambo JKT zilishuka daraja kwa pamoja.

Morogoro. Baada ya kupanda daraja viongozi wa Coastal Union SC wametakiwa kuweka mikakati ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao.
Coastal Union imepanda daraja baada ya kuifunga Mawenzi Market kwa mabao 2-0, shukrani kwa magoli ya kiungo Athman Idd ‘Chuji’ na Raizin Hafidh katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi B katika ligi daraja la kwanza.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Coastal Union iweke malengo na mikakati ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao.
Waziri Ummy alisema kitendo cha Coastal kurejea Ligi Kuu kimewapata faraja wana Tanga kwani ujio wa Simba, Yanga, Azam FC, Mtibwa Sugar na timu nyingine itatisha wananchi wa Tanga kuinuka kiuchumi.
“Licha ya Simba, Yanga, Azam FC na timu nyingine wakazi wa Tanga watapata fursa ya kufanyabiashara kwa wapenzi wa soka wataoingia kwenye jiji hilo, lakini sisi viongozi ngazi mbalimbali tupo tayari kuisapoti Coastal ili iweze kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu ujao.
Mbunge wa jimbo la Tanga Mjini, Alhaji Mussa Mbaruk akatoboa siri ya Coastal Union kurejea ligi kuu.
Alhaji Mbaruk alisema wanaitaka Coastal Union kuweka mikakati mapema ya kuandaa timu yenye ushindi zaidi ili iweze kufanya vizuri katika ligi hiyo msimu ujao kwani kiu ya wananchi wa Tanga kuona inatwaa ubingwa.
Alhaji Mbaruk alisema wanataka kuona Coastal Union ya  kushindana na hawako tayari kuona Coastal Union ya kushiriki lengo likiwa ni kubadilisha historia na kinyume cha hapo Coastal Union itatumbukia kwenye shimo.
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema kazi kubwa ilikuwa kuipandisha timu wamefanikiwa hivyo kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania bara msimu ujao.