Ngoma aipa masharti Simba

Muktasari:

  • Hivi karibuni kulikuwepo na tetesi za staa huyo kuletewa ofa na Pyramid, Al Alhy na Raja Casablanca, ila alitaka maombi hayo yapelekwe kwa uongozi wa Simba, kutokana na kuwa na mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Simba.

KIUNGO mkabaji wa Simba, Fabrice Ngoma amewapa masharti uongozi wa klabu hiyo, kama wanataka aendelee kusalia kikosini hapo, wasajili wachezaji wenye moyo wa kuipambania timu.

Hivi karibuni kulikuwepo na tetesi za staa huyo kuletewa ofa na Pyramid, Al Alhy na Raja Casablanca, ila alitaka maombi hayo yapelekwe kwa uongozi wa Simba, kutokana na kuwa na mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Simba.

Habari kutoka ndani ya uongozi wa klabu ya Wanamsimbazi zinasema,walikaa na staa huyo mezani,kujua anahitaji kitu gani ili aweze kubaki,ndipo alipotaja vitu viwili muhimu.

“Alisema anataka kuona Simba inachukua mataji, hivyo tusajili wachezaji wenye moyo wa kujituma na uchungu na timu,” alidokeza kiongozi huyo na kuongeza;

“Amesisitiza anaona ndani ya kikosi hicho ameona wachezaji wachache wa kigeni ndio wenye moyo wa kuipambania timu,jambo linalomuumiza kuona wakati anarejea mapumziko nchini kwao anakuwa hana furaha,”aliongeza.

Alisema hakuna mchezaji anapenda kucheza timu ambayo haina mafanikio kama kutwaa mataji na kufikia malengo ya mwanzo wa msimu kama wanavyokubaliana.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa kiungo huyo alitua Simba kutokana na mafanikio makubwa waliyoyapata ndani ya misimu minne mfululizo ambayo timu hiyo ilitwaa mataji mfululizo na kuwa na mafanikio kimataifa.

“Mchezaji anapenda mafanikio anapenda timu ipate mataji ishiriki michuano ya kimataifa na aliamini kuwa akiwa ndani ya Simba atapata mwanya wa kutoka hapo na kwenda kujaribu maisha mengine kutoka nje.” Kilisema chanzo hicho.