Simba wajiunga kupinga ubaguzi wa rangi
Muktasari:
Klabu ya Simba imekuwa timu ya kwanza nchini kutumia alama kama ishara ya kupinga ubaguzi wa rangi kutokana na kifo cha Floyd ambacho kimesababisha maandamano makubwa Marekani na kuzua taharuki duniani kote.
ASUBUHI ya leo Simba wameungana na klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya ikiwemo Chelsea na Liverpool kupinga tukio la ubaguzi wa rangi na mauaji ambayo alifanyiwa Mmarekani mweusi George Floyd, Mei 25 huko Minnesota na Polisi wa nchi hiyo.
Kabla ya kuanza kwa mazoezi ya leo asubuhi, wachezaji wa Simba, wametengeneza alama ya kupiga goti moja ikiwa ni ishara ya kutoa ujumbe wa kutaka haki itendeke kwa watu wote pasipo ubaguzi wowote wa rangi.
Wachezaji hao wa Simba, walipangwa na wasimamizi wao ili kupata umbo ambalo lilibeba ujumbe wa kupinga ubaguzi wa rangi wa 'imetosha sote ni binadamu'.
Tofauti na Chelsea ambao walitengeneza alama H wakiwa na maana ya 'Humans' kwa Simba haikuwa hivyo kwani kila mchezaji alitakiwa awe sehemu ya ujumbe bila kuzingatia kuchora kama ilivyokuwa kwa klabu nyingine.
Wachezaji wa Liverpool wenyewe walizunguka mduara wa kati kati ya uwanja na kupiga goti, ikiwa na maana sote ni binadamu tunapaswa kuwa wamoja.
Floyd ambaye ni raia mweusi wa Marekani ambaye kifo chake kimesababisha maandamano makubwa Marekani, alikufa kutokana na ukosefu wa hewa safi kwa mujibu wa uchunguzi wa maiti yake.
Alifariki kwa kukandamizwa kwa goti shingoni na mgongoni na maafisa wa polisi wa Minnesota, uchunguzi wa kimatibabu uliosimamiwa na familia ya Floyd umebaini hilo.