Simba kamili hiyoo bondeni

Friday July 12 2019

 

By Thobias Sebastian

HUKO Msimbazi kumekucha kwani mabosi wa klabu hiyo wamepanga timu yao ya Simba iondoke nchini wiki ijayo ili kwenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya Afrika Kusini kabla ya kurejea nchini Agosti 5 kuwahi tamasha lao la Simba Day.

Lakini wakati mabosi hao wakianza kuwapokea nyota wao ili kwenda Sauzi, nyota mmoja wa kigeni ambaye amepangwa kusajiliwa ili kukamilisha usajili wa watetezi hao wa Ligi Kuu Bara, amedaiwa kuwagawa vigogo wa Msimbazi, ingawa haijawa ishu sana.

Ni hivi. Vigogo wa klabu hiyo wamegawanyika juu ya nyota wa nafasi gani wamsajili kati ya beki wa kulia wa kumsaidia Shomari Kapombe ama mshambuliaji wa kuongeza nguvu kule mbele na mwishowe wote wakakubali bora aje straika na ikishindikana watauchuna hadi dirisha dogo kwa sababu kwa sasa Msimbazi kuna majembe ya maana.

Hata hivyo, katikati ya mchongo huo wa kumalizia usajili imebainika kuwa kikosi kizima cha Simba kikiongozwa na kocha wao, Patrick Aussems kitaondoka nchini kati ya Julai 14-15 kwenda Afrika Kusini, japo uongozi umeshindwa kuweka bayana watafikia mji gani.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema watakwenda kuweka kambi katika eneo lenye hali ya hewa na mazingira mazuri yatakayoruhusu maandalizi ya msimu kama ilivyokuwa msimu uliopita walipoiweka Uturuki.

Magori alisema kuna utaratibu wa kiutawala katika eneo ambalo wanataka kwenda kwa kuwa kuna malipo ambayo wanamalizia kulipa kisha baada ya hapo ndio watakuwa na uhakika wa kwenda katika nchi na mji huo, na baada ya hapo ndio watautangaza.

Advertisement

“Tutaondoka alfajiri ya Jumapili kwenda kambini tukiwa na nyota wote wapya na wale waliokuwapo msimu uliopita, benchi la ufundi na viongozi ambao watakuwa viongozi wa msafara na kambi hiyo ya zaidi ya wiki mbili,” alisema.

Magori alisema wana chaguo la nchi tatu kwenda kuweka kambi, lakini Afrika Kusini imekuwa chaguo la kwanza na kama itatokea mabadiliko basi wataweka kila kitu hadharani Jumamosi ili kuwahabarisha umma wa wana Simba wataenda wapi na watafikia mji gani.

Mratibu wa klabu hiyo, Abbas Seleman alisema wanatarajia kuwapokea makocha wao kuanzia leo Alhamisi ili kabla ya safari yao kila kitu kiwe sawa, huku Meneja Patrick Rweyemamu akisema taratibu za wachezaji na makocha kuwasili ziko sawa. Kwenda kwao kambini nchini Afrika Kusini kutakuwa ni marudio ya msimu wa 2017-2018, Simba ilipoenda kujichimbia mji wa Johannesburg mwaka 2017 kabla ya mwaka jana kuamua kukimbilia Uturuki ambapo hata hivyo hali ya hewa ya mvua ilivuruga programu ya Kocha Patrick Aussems.

NYOTA AWACHANGANYA

Katika hatua nyingine, mabosi wa Simba wamegawanyika juu ya nyota gani wa kigeni wamchukue wakati wakielekea kukamilisha usajili wao kwa msimu ujao, hasa baada ya kumtambulisha Gadiel Michael akiwa miongoni mwa waliokuwa wakiwahitaji.

Mmoja wa vigogo wa Simba aliliambia Mwanaspoti kuwa kulikuwa na ubishani kati ya beki wa kumsaidia Kapombe ama straika wa kigeni ndiye afunge usajili wa Msimbazi na wengine wakitaka nafasi hiyo iachwe wazi kwa ajili ya dirisha dogo.

“Kikao chetu cha mwisho kabla ya timu kuondoka hapa nchini Jumapili tutapata uamuzi wa mwisho kama tumsajili, kwani tuna majina matatu au tuiache wazi. Iwapo tutamsajili maana yake tutalazimika kulipa faini iliyotangazwa na CAF kupitia TFF,” alisema kigogo huyo, lakini Magori alipotafutwa alikiri ni kweli Simba haijamaliza kusajili.

“Tukikamilisha usajili wa mchezaji huyo wa kigeni ndio tutafunga usajili katika timu yetu msimu huu, lakini kwa sasa bado tupo kwenye mazungumzo,” alisema Magori bila kutaja mchezaji huyo ni yupi, japo Mwanaspoti linafahamu ni straika kutoka Zambia.

Advertisement