Simba, Yanga wataweza kweli?

Wednesday September 30 2020

 

By ELIYA SOLOMON NA THOMAS NG’ITU

BADO mechi mbili za Ligi kufikia mchezo wa watani wa jadi, Oktoba 18 lakini akili zote za mashabiki zinaonekana kugeukia huko kuanzia mitaani mpaka kwenye mitandao ya kijamii.

Mashabiki wanausubiri mchezo huu kutokana na timu zote kufanya usajili wa maana ambao, unawaruhusu kumfanya kila shabiki kusimama kifua mbele akijivunia kikosi chake bila shaka.

Kuelekea katika mchezo huo kila timu tayari imeshacheza mechi nne huku wakishinda mechi tatu kila mmoja na kutoka sare mchezo mmoja mpaka sasa.

Lakini, pamoja na tambo za timu hizo, wadau wamedai ubora wa timu walizokutana nazo ni wakawaida ingawa wamesifia uwezo wa Simba kutengeneza nafasi nyingi na kufunga mabao mengi kuliko Yanga.

Mjadala mkubwa wa kiufundi umekuwa ni kwamba timu zote zilizofungwa na Simba na Yanga, hazina mshambuliaji wala mchezaji yoyote mwenye goli mbili kwenye ligi mpaka sasa kwani wote wana bao moja moja tafsiri ambayo inaibua pia udhaifu wao na kwamba, bado hazijajipanga vizuri na wala matokeo si kigezo cha ubora kwa watani hao.

SIMBA

Advertisement

Simba mpaka sasa wamefunga magoli 10 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara mbili tu na wakijikusanyia pointi 10 katika mechi nne.

Kikosi cha Simba ambacho kinatumia mfumo wa 4-2-3-1 kuanzia eneo la viungo mpaka ushambuliaji limekuwa tishio kwelikweli katika Ligi Kuu Bara.

Viungo Clatous Chama, Bernard Morrison, Mzamiru Yassin na Luis Miquissone wamechangia upatikanaji wa mabao kwa hali ya juu kwani, wote kufunga kwa wakati tofauti au kutoa pasi za mabao.

Chama mpaka sasa ameifungia timu hiyo magoli mawili katika mchezo wao dhidi ya Biashara United ulioipa Simba ushindi wa mabao 4-0 huku Luis akihusika kutengeneza nafasi tatu za mabao kwenye mchezo huo.

Luis alitengeneza nafasi zote za mabao kwa Chama na lile la tatu ambalo alimpigia pasi Meddie Kagere akiwa ndani ya boksi na kufumua shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Kiungo ambaye hajapata nafasi sana ya kuanza katika kikosi cha Simba, Bernard Morrison mpaka sasa amehusika katika magoli mawili ya Chris Mugalu katika mchezo dhidi ya Biashara, baada ya kiungo huyo kuanzisha mashambulizi akitokea pembeni na kupiga pasi kwa Chama aliyempigia pasi ya kisigino Mugalu na kufunga.

Morrison pia alihusika katika bao la pili msimu huu kwa Mugalu katika mchezo dhidi ya Gwambina, baada ya kutokea pembeni na kupiga pasi mpenyezo kwa Mugalu, ambaye alitupia moja kwa moja wavuni.

Mzamiru naye amekuwa bora msimu huu akionyesha kiwango bora eneo la kati, pia ameifungia Simba mabao mawili dhidi ya Ihefu katika ushindi wa 2-1 na Mtibwa Sugar ulioisha kwa sare 1-1.

Huko kwa washambuliaji licha ya Kagere kutajwa yuko katika kiwango cha kawaida, mpaka sasa ameifungia Simba mabao mawili dhidi ya Biashara na Gwambina akiunganisha kichwa kona ya Luis.

Naye Mugalu licha ya kwamba hajapata nafasi ya kuanza mara kwa mara msimu huu, ameitumia vizuri nafasi ndogo anayopata baada ya ya kufunga magoli mawili kwenye mechi tofauti, moja akifunga dhidi ya Biashara na Gwambina zote zikiwa asisti za Morrison.

Nahodha John Bocco ameifungia timu yake bao moja dhidi ya Ihefu.

Hata hivyo, kwa upande wa mabeki Simba, Kocha Sven aliamua kumuondoa kikosini Kennedy Juma na kumuingiza Pascal Wawa baada ya mechi mbili za mwanzo na kuwa miongoni mwa kikosi kilichoruhusu mabao mawili tu.

Sven anawatumia Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Joash Onyango na Wawa katika mechi mbili za mwisho na hawakuruhusu nyavu kuguswa tofauti na mechi mbili za mwanzo ambazo kwenye safu hii alikuwepo Kennedy.

YANGA

Ukiiondoa Azam FC ambayo haijaruhusu bao hata moja msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Yanga na Ruvu Shoooting ndio zimeonekana kuwa imara katika ulinzi.

Klabu hizo mbili zimeruhusu bao moja tu. Yanga wao waliruhusu bao hilo dhidi ya Tanzania Prisons katika sare ya bao 1-1.

Ukuta wa Yanga ambao uliruhusu bao hilo, ulikuwa ukiongozwa na kipa Farouk Shikalo huku mabeki wake wakiwa Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Bakari Mwamnyeto.

Bao ambalo alifungwa Shikalo katika mchezo huo, lilikuwa shuti matata la Lambart Sabiyanka akiwa nje ya eneo la hatari na kuwatanguliza Wajelajela. Yanga walisawazisha kupitia kwa Michael Sarpong baada ya kazi nzuri ya Farid Mussa.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic alifanya mabadiliko kadhaa kwa kuanza kuwatumia, kipa Metacha Mnata, Lamine Moro, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda na Carlinhos, ambaye awali alionekana kutokuwa fiti.

Tangu Septemba 13, mwaka huu, Yanga haijaruhusu bao katika mechi dhidi ya Mbeya City kisha Kagera Sugar na kumalizia na Mtibwa Sugar pale Jamhuri.

Katika mechi zote hizo, Yanga iliondoka na ushindi wa 1-0 kwenye kila mechi na kuvuna alama tisa huku mechi mbili ikicheza ugenini (Kaitaba-Bukaba na Jamhuri-Morogoro).

Kati ya ushindi huo wa Yanga, Lamine ndiye ameonekana kuibeba akifunga dhidi ya Mbeya City kisha Mtibwa Sugar huku lingine likifungwa na Mukoko. Lamine, ambaye ni mhimili mkuu kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, amefunga mabao ndiye mawili katika mechi tatu za Yanga.

Mabao hayo yameiwezesha Yanga kuvuna pointi sita kwenye michezo hiyo huku lile la Mukoko likiibeba Yanga pale uwanja wa Kaitaba dhidi ya Kagera Sugar waliokuwa nyumbani.

Mpaka sasa wachezaji wa Yanga waliohusika kwenye mabao hayo manne ni Lamine, Mukoko na Sarpong kwa msaada wa asisti za Carlinhos na Farid, ambaye katika mechi za karibuni amekuwa benchi.

Carlinhos amehusika katika mabao mawili dhidi ya Mtibwa na Mbeya City huku Kisinda akihusika dhidi ya Kagera.

Yanga imesaliwa na michezo miwili ambayo ni dhidi ya Coastal Union ya Tanga na Polisi Tanzania kabla ya kuvaana na watani zao wa jadi, Simba ambao wameonekana kuwa tishio kwenye upachikaji mabao huku wakiruhusu nyavu zao kuguswa mara mbili.

Hata hivyo, itategemea mabadiliko ya ratiba ambayo yatapanguliwa hivi karibuni na TFF.

MECHI ZIJAZO SIMBA

JKT TZ v Simba

Prisons v Simba

Simba v Yanga

MECHI ZIJAZO YANGA

Yanga v Coastal

Yanga v Polisi TZ

Simba vs Yanga

Advertisement