Simba, Yanga mtihani mgumu mechi za ugenini

Muktasari:

Yanga inayoongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 74, itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Dar es Salaam. Wakati Yanga leo inacheza na Mtibwa Sugar, Simba itaanza kucheza mechi zake za viporo dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Yanga inayoongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 74, itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Rekodi inaonyesha Coastal Union itakuwa na kazi ngumu kwa kuwa tangu mwaka 2013 zilipokutana katika mechi tatu kwenye uwanja huo, Simba imeshinda moja na imetoka sare mara mbili. Katika Uwanja wa Taifa, Simba imeshinda mechi mbili na kutoka sare mara moja.

Kwa upande waYangarekodi inaweza kuibeba kwa kuwa tangu mwaka 2015 katika mechi nne ambazo timu hizo zimekutana imeshinda mara mbili, Mtibwa  mara moja na zimetoka sare moja.

Akizungumza kwa simu jana, Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alisema Mtibwa ni timu bora ina kikosi chenye ushindani, lakini watapambana kupata pointi tatu.

Baada ya Simba kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe ya DR Congo imebakiwa na mechi 16 zikiwemo mechi 11 za viporo 11 ambavyo leo itaanza kuvipunguza.

Simbaimebakiwa na mechi dhidi ya KMC, JKT Tanzania Biashara United (mechi mbili),Mtibwa Sugar(Mechi  mbili),Coastal Unon (mechi mbili), Kagera Sugar (mechi mbili), Alliance FC,

Prisons, Mbeya City, Azam, Ndanda na  Singida United.

Mechi tisa kati ya hizo itacheza ugenini  dhidi ya KMC, Coastal Union, Kagera Sugar, Alliance,Biashara United, Prisons, Mbeya City, Singida United na Mtibwa Sugar. Mechi saba za nyumbani dhidi ya JKT Tanzania,  Biashara United,Mtibwa Sugar,Coastal Union, Kagera Sugar,Azam, Ndanda.

Katika mechi 16 ambazo Simba itapata na kazi ngumu dhidi ya Prisons ya Mbeya inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 42.

Tangu mwaka 2013 zimepepetana mara tano kwenye Uwanja wa Sokoine na Simba imeshinda mara moja, Prisons imeshinda mechi mbili na zimetoka sare mara mbili.

Akizungumza jana, Kocha wa Prisons,Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Simba isitegemee mteremko kwa kuwa amekiandaa kikosi cha ushindi.

“Tunataka tuendeleze rekodi yetu bora kwenye uwanja wetu dhidi ya Simba na  tunaomba Mungu atuwezeshe kushinda hatutaki sare ni ushindi, ”alisema Rishard.

Pia Simba inaweza kupata taabu dhidi ya  Azam Mei 12 kwa kuwa wapinzani wao  

wako katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Tangu mwaka 2015 timu hizo zimekutana mara tisa, Simba imeshinda mechi nne, sare nne, Azam imeshinda mechi moja tu na mara ya mwisho Azam kuifunga Simba katika Ligi Kuu ni Machi 30, 2014 iliposhinda mabao 2-1.

Mechi dhidi ya Kagera Sugar, Simba imekuwa na rekodi nzuri, katika mechi nne kwenye Uwanja wa Kaitaba tangu mwaka 2015 imeshinda mara tatu na kupoteza moja matokeo ambayo ni sawa na mechi nne ilizocheza Uwanja wa Taifa.

Hata hivyo, Simba msimu wa 2016/2017 ilitibuliwa ubingwa wake baada ya Aprili 12, 2017 kuichapa Simba mabao 2-1 na kuiacha Yanga ikitwaa taji hilo.

Timu nyingine ambayo Simba ina uhakika wa kupata pointi ni Ndanda ambayo haijawahi kuifunga Simba kwenye Uwanja wa Taifa wala Nangwanda Sijaona, Mtwara. Katika mechi tatu tangu mwaka 2016 Simba imeshinda zote.

Singida United United inayoshika nafasi ya 10 kwa pointi 40, imefungwa mechi zote tatu nyumbani na ugenini, hivyo rekodi inaibeba Simba katika mchezo wao wa Mei 22.

Pia Mbeya City, JKT Tanzania zimekuwa zikifungwa mara nyingi na Simba hivyo inaweza isipate kazi kubwa kwani tangu mwaka 2015 imekutana na timu hizo mara nne nyumbani na ugenini na kila mmoja ameifunga Simba mechi moja tu.

Mtibwa Sugar haifui dafu mbele ya Simba kwani tangu mwaka 2016 katika mechi sita ambazo timu hizo imekutana ugenini imeshinda mechi mbili na kutoka sare moja wakati nyumbani pia katika mechi tatu imeshinda mbili na sare moja.

Mara ya mwisho Mtibwa Sugar kuifunga Simba ilikuwa msimu wa 2012/2013 iliposhinda mechi zote  mbili, iliichapa mabao 2-0 kabla ya kushinda 1-0.

Mchambuzi Ally Mayay alisema kutokana na kiwango cha Simba ilichokionyesha kwenye mashindano ya kimataifa ana uhakika watafanya vizuri katika mechi zao zote zilizobaki za Ligi Kuu.

“Hata kama watacheza mechi moja kwenda nyingine kila baada ya saa 72 bado watafanya vizuri kwa sababu  Ligi ya Mabingwa Afrika imewapa mazoezi na uzoefu mkubwa,”alisema Mayay.