Simba, Yanga kucheza saa 8:00 mchana

Muktasari:

Kwa mujibu wa Afisa habari wa TFF, Cliford Ndimbo alisema muda wa mechi umebadilishwa kutoka saa 10:00 mpaka saa 8:00.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),limerudisha nyuma muda wa mechi hizo, sababu zikisemekana ni uwepo wa michuano ya AFCON kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 inayoendelea Tanzania wakiwa wenyeji.
TFF imetoa tariha hizo leo siku moja kabla ya mechi hizo za kesho ambapo Simba na Yanga zote zinacheza ugenini.
Kwa mujibu wa Afisa habari wa TFF, Cliford Ndimbo alisema muda wa mechi umebadilishwa kutoka saa 10:00 mpaka saa 8:00.
Mbali na taarifa za kurudishwa muda nyuma wa kucheza mechi hizo, makocha wa timu hizo wamezungumzia maandalizi na maoni juu ya mechi hizo.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems anasema Coastal Union sio timu ya kuibeza hivyo wamejipanga kuhakikisha wanashinda mechi hiyo "Itakuwa mechi ngumu na wachezaji wanalitambua hilo na wameahidi ushindi"anasema.

Naye Juma Mgunda kocha wa Coastal Union ya Tanga anasema "Simba wana malengo yao ya kupigania ubingwa, lakini pia na wao wana malengo yao ya kujiweka nafasi nzuri.
"Itakuwa mechi ya ushindani, dakika 90 ndizo zitakazoamua nani alikuwa na mbinu dhidi ya mwenzake"anasema.
Huko Morogoro, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera anasema wachezaji wake wana morali ya kushinda mechi za mikoani hivyo Mtibwa Sugar hawatawaacha salama.
Zuber Katwila kocha wa Mtibwa Sugar amejibu mapigo kwamba hata kama Yanga waliwafunga mzunguko wa kwanza mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Jamhuri wasitegemee mtelemko.