Cheki jinsi Simba SC ilivyoipiga bao Yanga

Muktasari:

iaka ya hivi  karibuni nyota mbalimbali wa soka Tanzania bara wamekuwa wakichomoka mmoja mmoja kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa lakini timu ya Simba imeonekana kuwa na bahati ya wachezaji wengi kuliko timu kama Yanga na Azam.

SIMBA noma sana, kwani unaambiwa mipango yao ya kunasa mkwanja haijaanza leo.

Si mnajua kwa miaka ya karibuni nyota mbalimbali wa soka wamekuwa wakichomoka mmoja mmoja kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa? Lakini unaambiwa wimbi hilo limezidi baada ya Mbwana Samatta kuchomoka TP Mazembe na baadaye Genk ya Ubelgiji.

Zamani wachezaji wengi wa Bongo hawakuwa na habari ya kwenda nje ya nchi kusaka ulaji na badala yake wengi walikuwa waking’ang’ania kucheza ligi za hapa pekee.

Kuna baadhi walienda na kurudi kama Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye alisajiliwa na Gefle IF ya Sweden, japo hakukaa kwa kipindi kirefu kwa kile kilichoelezwa hakuwa tayari kukatwa kodi kutoka kwenye mshahara wake uliotajwa kuwa Dola 5,000 kwa mwezi.

Lakini sasa tangu wimbi hilo lianze klabu ya Simba imeonekana kuwapiga bao wapinzani wao Yanga katika kuuza wachezaji nje ya nchi.

Hata hivyo kwa kuchukua hesabu za haraka za kuuza wachezaji ndani ya miaka mitano ni kwamba Azam ndio kinara, ila kwa watani wa jadi Simba imefunika kinoma kwa kuvuta mkwanja.

Wapo wengine pia wamekuwa wakitimkia nje kufanya majaribio au kujiunga kabisa na timu za huku kwa lengo la kupata pesa, pia kuibeba timu ya Taifa ya Taifa, Taifa Stars.

Ndani ya miaka mitano wachezaji 10 walisajiliwa na klabu za nje kutoka Simba, Yanga na Azam huku wanne wakiishia kufanyia majaribio.

Wachezaji wanane kutoka katika klabu hizo tatu wamesajiliwa na klabu za Afrika wakati wawili wakisajiliwa Ulaya huku sita wakicheza katika Ligi Kuu na wawili wakiwa Ligi Daraja la Kwanza.

Kwa miaka mitano katika timu hizo tatu, Azam imeonekana kutisha zaidi kwani wachezaji wake wengi wamesajiliwa na klabu za nje (wanne) ikifuatiwa na Simba (watatu) na Yanga (watatu), Azam imewatoa Farid Mussa, Shaaban Idd Chilunda waliosajiliwa na klabu ya Ligi Daraja la Kwanza ya CD Tenerife ya Hispania, Himid Mao (Petrojet, Misri ) na Yahya Zayd Ismailia ya Misri.

Waliosajiliwa wakitokea Simba ni Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Shiza Kichuya (Pharco FC/ENPPI, Misri) na Emmanuel Okwi ambaye hata hivyo alivunja mkataba na Klabu ya SonderjyskE ya Sweden na sasa yuko katika kikosi cha Simba.

Yanga ilimuuza Simon Msuva (Difaa El Jadida) pia wapo waliondoka wakiwa huru kama Hassan Kessy (Nkana Red Devils) na Mrisho Ngassa (Free State ya Afrika Kusini) mwaka 2015.

FEDHA

Timu nyingi zimekuwa zikifanya siri zinapouza wachezaji huku habari zikidai zinaogopa watu wengi kujitokezan kutaka mgao wa fedha hizo wakiwemo mawakala wa wachezaji, timu walizochezea wakiwa wadogo na pia makato ya kodi.

Simba imeonekana kuvuna pesa ndefu zaidi ikiwa imepata zaidi ya sh 445 milioni kwa kuwauza Okwi na Kichuya pekee huku Abdi Banda akiondoka kama mchezaji huru. Yanga ilivuna Dola 100,000 sawa na Sh 230 milioni kwa kumuuza Msuva.

Azam inaweza ikawa ndio timu iliyovuna pesa ndefu zaidi, lakini usajili wa wachezaji wake wanne umefanywa siri na kugoma kutaja kiasia walichopata.

WACHEZAJI WENYEWE

Abdi Banda

-Baroka FC

Beki huyu wa kati anayemudu pia kucheza beki za pembeni pia aliondoka kama mchezaji huru Julai mwaka 2017 na kujiunga na Baroka FC ya Afrika Kusini.Mchezaji bado alikuwa akitakiwa na Simba, lakini licha ya uongozi kufanya naye mazungumzo aligoma na kwenda kutafuta changamoto nyingine.

Emmanuel Okwi

Mganda huyu ndiye mchezaji pekee ambaye ameiingizia Simba kiasi kikubwa cha pesa akiwa ameipatia jumla ya Dola 410,000 zaidi ya Sh946 milioni akiwa na timu mbili tofauti.

Simba ilimuuza Okwi kwa Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013 kwa Dola 300,000 zaidi ya Sh600 milioni.

Hata hivyo, alivunja mkataba huo na kurejea SC Villa ya Uganda na kisha kujiunga Yanga.

Hakumaliza msimu Yanga na kisha kutimkia Simba na mwaka 2015 Wekundu wa Msimbazi wakamuuza katika klabu ya Sonderjyske ya Sweden kwa Dola 110,000 zaidi ya Sh 250 milioni.

Shiza Kichuya- Pharco

Ameuzwa klabu ya Daraja la Pili ya Pharco ya Misri kisha kutolewa kwa mkopo katika timu ya ENPPI inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.

Kichuya amesajiliwa na klabu hiyo kwa dau la Dola 85,000 sawa na Sh 195 milioni.

Msuva- Difaa El Jadida

Yanga ilimuuza winga wake mahiri, Simon Msuva kwa Difaa El Jadida ya Morocco mwaka 2017.

Inadaiwa timu hiyo ilimuuza Msuva kwa Waarabu hao kwa Dola 100000 sawa na sh 230 milioni.

MRISHO Ngassa - Free State

Mei 2015 Yanga ilimuacha winga wake, Mrisho Ngassa ajiunge huru kwa klabu ya Free State ya Afrika Kusini.

Awali Free State ilitaka kuipa Yanga Dola 80,000 lakini ikakataa ikitaka ipewe Dola 150,000 lakini mwisho mkataba wa Ngassa ukamalizika Jangwani hivyo akajiunga bure katika klabu hiyo ya Afrika Kusini.

Hata hivyo, mchezaji huyo aliichezea timu hiyo msimu mmoja kabla ya kuamua kuvunja mkataba kwa makubalino na klabu yake na kurejea nchini.

Kabla ya kurudi Yanga, Ngassa alizechezea Mbeya City na Ndanda FC.

Hassan Kessy- Nkana

Mchezaji mwingine aliyetokea Yanga na kujiunga na klabu ya Nkana Red Devils ya Zambia kama mchezaji huru.

Yanga ilifanya mazungumzo na Kessy ili aongeze mkataba mpya lakini beki huyo aligoma kwa madai hawakuwa tayari kumpa kile alichotaka, hivyo akaamua kuondoka na kujiunga na Nkana ambao inasemekana ilimpa Sh 70 milioni.

Farid Mussa - CD Tenerife

Azam FC ilimtoa kwa mkopo mshambuliaji wake Farid Mussa kwa klabu ya CD Tenerife ya Hispania.

Farid amejiunga na CD Tenerife mwaka 2016 kwa mkataba wa miaka miwili na inasemekana ameongeza mkataba mwigine wa miaka miwili hivi karibuni.

Shaaban Idd - CD Tenerife

Mchezaji huyu naye alitolewa kwa mkopo na Azam katika timu ya CD Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania mwaka jana.

Idd anakuwa mchezaji wa pili kujiunga na timu hiyo akitokea Azam baada ya Farid Mussa.

Himid Mao - Petrojet

Azam iliendeleza moyo wake wa kutowabania wachezaji wake kujiunga na timu za nje baada ya Juni mwaka jana kumruhusu kiungo wake mkabaji Himid Mao kujiunga na klabu ya Petrojet ya Misri.

Himid amejiunga na Petrojet kwa mkataba wa miaka mitatu utakaomalizika mwaka 2021.

Hata hivyo, Azam haijataja dau ililomuuza kiungo huyo kwa madai ni siri yao.

Yahya Zayd -Ismailia.

Kama kawaida Azam ikafungua mwaka mpya kwa kumuuza mshambuliaji wake, Yahaya Zayd kwa klabu ya Ismailia ya Misri.

Ismailia imempa Zayd mkataba wa miaka mitatu moja kwa moja bila kumfanyia majaribio kama wachezaji wengine.

WACHEZAJI WA MAJARIBIO

Jonas Mude

Kiungo mahiri wa Simba, Jonas Mkude amewahi kufanya majaribio na klabu za Bidvest Wits na Mpumalanga zote Afrika Kusini mwaka 2015 kabla ya kurejea na kisha kwenda tena mwaka 2016 kufanya majaribio na Bidvest lakini hakusajiliwa huku sababu zikifichwa.

Said Ndemla -AFC Eskilstuna

Kiungo mshambuliaji Said Ndemla amekuwa akihusishwa mara kwa mara kwenda kufanya majaribio nje ya nchi hasa Sweden na kurejea huku kukiwa hakuna sababu za kushindwa kujiunga na timu hizo

Ndemla amewahi kufanya majaribio na klabu ya AFC Eskilstuna ya Sweden na inadaiwa hivi sasa yuko Sweden kufanya majribio na klabu hiyo hiyo huku Simba ikiwa tayari kumuachia.

Ibrahim Ajibu -Lamontville Golden Arrows FC

Mshambuliaji huyo aliyekwua akiichezea Simba ,mwaka 2016 aliwahi kwends Afrika Kusini kwa majaribio katika klabu ya Lamntville Golden Arrows FC inayoshirikiLigi Kuu.

Hata hivyo, Lamontville Golden Arrows FC haikuwa tayari kumnunua mchezaji huyo, bali ilitaka kumchukua kama mchezaji huru na kumsainisha mkataba.

Kwa sababu hiyo, klabu hiyo ilimuambia Ajibu arejee Dar es Salaam kuangalia kama mkataba wake umekwisha apeleke uthibitisho Afrika Kusini ingawa uongozi wa Simba ulikomaa na kusema bado Ajibu ana mkataba.

Ramadhani Singano - Difaa El Jadida

Mwaka 2017 Singano alitimkia Difaa El Jadida kufanya majaribio lakini akarejea nchini baada ya kufeli majaribio hayo.

Mpaka leo bado yupo Azam FC akijipanga upya na kuona kama atafanikiwa kupata dili lingine la kwenda kukipiga nje ya nchi na kuongeza idadi ya wachezaji wakitanzania wanaokipiga nje na kuzidi kuvuta pesa ndefu.