Mechi ya Simba vs Yanga burudani tosha!

Muktasari:

Kwa kuangalia vikosi vyote viwili ni kwamba ni timu zenye nyota wenye uwezo wa kuamua matokeo ya mchezo huo ndani ya dakika 90, huku wakibebwa na rekodi tamu za makocha walionao.

MAONI YA MHARIRI

ZILE tambo, kejeli na mikwara iliyorindima ndani ya wiki nzima kutoka kwa wadau wa klabu kongwe za Simba na Yanga zinafikia tamati jioni ya leo wakati Simba na Yanga zitakapovaana jijini Dar.

Timu hizo zitakutana kwenye pambano lao la 102 katika mechi za kuwania ubingwa wa Bara tangu ilipoasisiwa mwaka 1965, ukiwa ni wa marudiano kwao baada ya mechi yao ya kwanza kutotoa mshindi.

Katika mechi yao ya kwanza kwa msimu huu wa 2018-2019 iliyochezwa Septemba 30 mwaka jana, timu hizo zilitoka suluhu licha ya tambo na mikwara na iliyoanikiza wiki nzima sasa.

Hili ni pambano linalovuta hisia za watu wengi na linalofuatuliwa ndani na nje ya nchi kutokana na upinzani wa jadi uliopo baina ya timu hizo zilizoasisiwa zaidi ya miaka 80 iliyopita.

Simba na Yanga ni kati ya klabu kongwe barani Afrika na ambazo zimemudu kuwepo katika Ligi Kuu kwa miaka mingi bila kushuka daraja, lakini pia zikiwa ndizo zilizotwaa mataji mengi nchini.

Tangu ilipotangazwa kwenye ratiba kuwa, klabu hizo zitarudiana Februari 16, 2019 kumekuwa na tambo, kejeli na majigambo toka kwa wanazi wa klabu hizo, kila upande ukitamba kuibuka na ushindi safari hii baada ya suluhu ya mechi ya kwanza.

Kwa kuangalia vikosi vyote viwili ni kwamba ni timu zenye nyota wenye uwezo wa kuamua matokeo ya mchezo huo ndani ya dakika 90, huku wakibebwa na rekodi tamu za makocha walionao.

Yanga inafundishwa na Kocha Mwinyi Zahera kutoka DR Congo aliyeiongoza timu hiyo kucheza mechi 23 ikishinda 18 kupoteza mmoja na kutoka sare michezo minne.

Watani wao walio chini ya Kocha Mbelgiji Patrick Aussems nao wamecheza mechi 15 mpaka sasa katika Ligi Kuu, wakishinda 11, huku tatu wakiambulia sare na mchezo mmoja kuupoteza.

Licha ya kutenganishwa kwenye msimamo, Yanga ikiwa kileleni na alama zao 58 na Simba kushika nafasi ya nne (kabla ya matokeo ya mechi za jana Ijumaa) wakiwa na pointi 36, lakini hazitofautiani.

Kutokana na hali hiyo ni wazi mashabiki wa soka watataka kwenda Uwanja wa Taifa leo kwa ajili ya kupata burudani na si kingine, hivyo nyota wa timu hizo wana wajibu wa kukata kiu yao.

Hatutarajii kulishuhudia pambano la kukamiana ama lenye kujaa ubabe na vituko vinavyoondoa maana halisi ya mchezo wa soka hasa kwa timu za watani wa jadi.

Muhimu ni kwa mwamuzi Hans Mabena aliyeaminiwa na kupewa fursa ya kulichezesha pambano hilo, alitendee haki na kufanya kila njia kulifanya pambano liendane na hadhi yake.

Tunaamini Mabena ni mmoja ya waamuzi makini na wanaotoa maamuzi yake uwanjani kwa kuzingatia sheria na kanuni za soka na ndivyo atakavyofanya leo kwenye pambano hilo la watani.

Kama waamuzi watatimiza wajibu wao kikamilifu na wachezaji nao wakacheza soka uwanjani ndani ya dakika 90 ni dhahiri wale wote watakaoenda Taifa watapata burudani na watakata kiu yao.

Soka ni burudani. Soka ni furaha na pia ni upendo na udugu, hivyo kila atakayehudhuria au atakayeshiriki kwa namna moja au nyingine katika pambano hilo ana wajibu wa kulizingatia hilo.

Kwa maana hata mashabiki watakaoenda uwanjani washangilie timu zao kwa ustaarabu na kuepukana na mambo yote ya ovyo ama vitendo vinavyouvunjia hadhi mchezo huo na kujidhalilisha.

Yale mambo ya mashabiki kujifanya wana hasira na kufanya kama yaliyojiri kwenye mchezo wa watani wa Oktoba Mosi, 2016 hatutarajii yajirudie kwa vile mtu hujifunza kutokana na makosa.

Tunazitakia kila la heri Simba na Yanga kwa kuamini aliyejipanga vyema ndiye atakayepata matokeo mazuri kwani kila mtu huvuna kile alichopanda na muhimu anayeshindwa aua kushinda aridhike.

Pia tunawatakia kila la heri waamuzi wautendee haki mchezo huo kama ambavyo tunavyoomba kwa mashabiki nao wautendee haki kwa kuhudhuria na kuzingalia timu zao kwa furaha na amani na baada ya dakika 90 ule utamaduni wa kutaniana bila kupigana uendelee kama kawaida kwa kuwa huo ndio utani wa jadi ulivyo.