Simba, Namungo mambo ni moto!

Wednesday July 29 2020

 

By Mussa Mwangoka, Sumbawanga

HAWATAKI mchezo! Namungo FC ya Lindi imekuwa ya kwanza kuwasili mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, ambapo iliwasili jana kimya kimya kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wa Fainali ya Kombe la  Shirikisho la Azam, mchezo utakachezwa katika uwanja wa Nelson Mandela mjini hapa.

Wakati Namungo wakiwasili kimya kimya na kufikia katika hoteli ya Kanisa la Moravian iliyopo katikati ya mji hapa, wapinzani wao katika mchezo huo Simba SC ya Dar es salaam imeendelea na mazoezi katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambako imeweka kambi kwa muda kujiandaa na mchezo huo wa fainali.

Kocha wa Namungo, Hatimana Thierry alisema kuwa wao wanafahamu ubora wa Simba kuelekea katika mchezo wao wa fainali ndicho kilichowafanya wawahi kufika mjini Sumbawanga ili waendelee kufanya maandalizi kikamilifu huku wakimudu kukabiliana na hali ya hewa ya baridi kali.

"Simba wana timu nzuri kila mtu anafahamu kuhusu hilo, lakini kwa kuwa na sisi tuna vijana wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka la kuvutia na kupata matokeo uwanjani kwa hiyo tumejiandaa kwa ajili ya kutoa burudani nzuri kwa wakazi wa mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani...... na kuhakikisha tunatimiza lengo letu la kuchukua ubingwa wa michuano ya Kombe la Azam" alisema Kocha huyo.

Timu ya Namungo  baada ya kuwasili mjini hapa, ilionekana ikifanya mazoezi katika uwanja wa Shule msingi Mazeozi uliopo pembezoni kidogo mwa mji wa Sumbawanga na kuzua gumzo kwa baadhi ya wadau wa Soka wa mji huo.

Ambapo awali moja ya gari la Matangazo la Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga lilikuwa likipita mitaani na kutangaza kwamba timu hizo mbili zingewasili julai 30 siku ya Alhamisi hivyo wapenda soka wajiandae kwenda kuzipokea.

Advertisement

Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Rukwa, Blassy Kiondo amesema wao pia wameshangaa stahili ya kimya kimya waliyoingia nayo Namungo katika mji huo, kwani walipata taarifa kuwa wanaingia Sumbawanga wakiwa mji mdogo wa Laela kilometa 100 kutoka mji hapa.

"Wametusaprizi aisee kwa ujio wao wa kimya kimya............ila walipofika hapa tumewapatia ushirikiano wa kadri walivyohitaji na timu imefikia hoteli ya Moravian Center iliyopo mjini hapa" amesema Kiondo.

Pia amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika kwa asilimia 90, bado vitu vidogo vidogo kama kuweka magoli na kuchora alama za uwanjani hivyo wadau wa Soka wasiwe na wasiwasi wowote kuelekea mchezo huo.

Ameongeza tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa ambapo kuna vituo mbalimbali vimetengwa kwa ajili ya kuuzia tiketi hizo ambazo zitauzwa Sh 20,000 kwa jukwaa kuu na mzunguko ni Sh 10,000 ambapo wamefanya hivyo wakilenga kuingiza watazamaji 20,000 huku uwanja ukiwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 35,000.

Kwa upande wa Katibu wa Tawi la Simba mkoa wa Rukwa, Lusungu Kihahi alisema tawi hilo limejipanga kikamilifu kuipokea timu yao pindi itakapoingia katika ardhi ya mkoa huo, ambapo amedai Simba itapokelewa na kundi la kwanza katika eneo la Mpakani mwa mkoa wa Rukwa na Songwe.

Kisha katika mji mdogo wa Laela ambako kutakuwa na kundi la pili la wanachama na kundi la tatu litakuwa katika kata ya Kaengesa kilometa 30 kutoka mjini Sumbawanga.

Advertisement