Sibomana ,Boxer warejesha mzuka Yanga

Tuesday October 15 2019

 

By Khatimu Naheka

YANGA imeanza kushusha presha baada ya wachezaji wake watano kurejea kazini tayari kujiandaa na mchezo dhidi ya Pyramid FC kwenye mechi ya mtoani kusaka nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Jana Yanga ilikuwa katika mazoezi na wakaialika Friends Rangers kama sehemu ya kujipima nguvu kushinda mabao 4-3, huku David Molinga akifunga mara mbili huku mengine yakifungwa na nahodha wao Pappy Tshishimbi na mshambuliaji Maybin Kalengo katika ushindi huo.

Wakati Yanga ikiwa katika mchezo huo huku nje ya uwanja kulikuwa na mashine tano ambazo zilikuwa zikifanya mazoezi mepesi.

Mashine hizo ni mabeki Lamine Moro, Paul Godfrey ‘Boxer’ winga mkongwe Mrisho Ngassa, Patrick Sibomana na Sydney Urikhob ambao walikuwa majeruhi na sasa wameanza kurejea wakianza na mazoezi mepesi ya viungo.

Wachezaji hao ni kati ya 12 ambao walikuwa katika orodha ya wagonjwa na kuwapa wakati mgumu mabosi wa Jangwani ambao akili zao wamezielekeza kwenye mechi dhidi ya Pyramid.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alisema hatua imeshusha presha ya benchi la ufundi na wanasubiri wachezaji hao kuwa fiti kamili.

Advertisement

Alisema kurejea kwa wachezaji hao ni hatua nzuri na imewapa faraja kubwa wakati huu wakijipanga kumkabili Mwarabu mchezo ambao amesema utakuwa mgumu.

“Unajua hakuna kocha asiyefurahi kuona wachezaji waliokuwa majeruhi wanarejea, hii ni hatua kubwa hasa kwa idadi yao.

“leo (jana) hawa watano wameanza na mazoezi mapesi na tunawafuatilia kwa karibu kuangalia uimara wao kama wataendelea kuimarika huku tukiwasubiri wengine, bado tuna muda wa kutosha kidogo kuweza kuwafuatilia,” alisema.

Msolla, mabosi wa ufundi wavamia

Wakiwa katika viwanja hivyo jana mabosi wa klabu hiyo wakiongozwa na Dk Mshindo Msolla walivamia katika mazoezi hayo na kufuatilia kile kilichokuwa kinafanyika.

Msolla alikuwa sambamba na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Salum Rupia aliyefuatana na wajumbe wake Abeid Mziba ‘Tekelo’ na Sunday Manara huku pia Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Saad Khimji akiwemo.

Msolla ameliambia Mwanaspoti anaridhishwa na ratiba na maandalizi ya timu yao yanavyoendelea na uongozi wake pia uko katika mipango ya ndani kuelekea mchezo huo.

Alisema kwa sasa wanasubiri ripoti kamili ya kocha wao, Mwinyi Zahera ambaye alikuwa nchini Ufaransa na timu yao ya taifa ya DR Congo ambayo juzi ilikubali kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Ivory Coast katika mchezo wa kirafiki.

“Maandalizi ni kama haya, hii nayo ni hatua nzuri kuwapa wachezaji kipimo, nimewaona vijana waliopo na waliocheza kuna kitu nakiona, huku kama uongozi tunaendelea kujipanga tukiwasubiri makocha watuambie wanachotaka, lakini pia nimeona kuna wachezaji aliokuwa majeruhi nao wamerejea na tunaendelea kupambana kuhakikisha wengine zaidi wanaimarika,” alisema Msolla.

Advertisement