Scholes ampa Ole chama la ushindi

Muktasari:

Man United imetinga hatua ya mtoano kwenye michuano hiyo ikiwa bado ina mechi mbili za kucheza kwenye kundi lake, ambapo mechi hiyo ya juzi Alhamisi usiku, washambuliaji wake wote aliowaanzisha, Mason Greenwood, Anthony Martial na Marcus Rashford walitikisa nyavu.

MANCHESTER, ENGLAND . SI unamfahamu Paul Scholes? Mkereketwa wa Manchester United, anayeumizwa kwelikweli timu hiyo inapofanya hovyo uwanjani.

Basi kuepuka matokeo ya kuumia, Scholes ametengeneza kikosi chake cha kwanza na kumwambia Kocha Ole Gunnar Solskjaer hicho ndicho kinachofaa kuanza kwenye kila mechi kama wanahitaji matokeo matamu baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Partizan Belgrade kwenye Europa League.

Man United imetinga hatua ya mtoano kwenye michuano hiyo ikiwa bado ina mechi mbili za kucheza kwenye kundi lake, ambapo mechi hiyo ya juzi Alhamisi usiku, washambuliaji wake wote aliowaanzisha, Mason Greenwood, Anthony Martial na Marcus Rashford walitikisa nyavu.

Scholes sasa anaamini kikosi bora cha Solskjaer kinaanza kupatikana, wakati timu hiyo ikiwa na shughuli pevu ya kupanda mlima huko kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikitambua imeshatinga kwenye hatua ya 32 bora ya Europa League.

Gwiji huyo wa Old Trafford alisema bado kuna swali zito la nani anayefaa kuwa patna wa Harry Maguire kwenye beki ya kati, lakini yeye anamwona Axel Tuanzebe anastahili kuanza ndipo atakapopona majeraha yake na hapo anampiga benchi Victor Lindelof. Kikosi hicho cha Scholes, anasema Paul Pogba atacheza na Scott McTominay kwenye kiungo, wakati Danie James, Rashford na Greenwood watacheza nyuma ya Martial kwenye fowadi. Mabeki wa pembeni wa Scholes ni Aaron Wan-Bissaka kulia na Luke Shaw upande wa kushoto.

“Ni 4-4-1-1 naiona kabisa kuwa ni fomesheni safi ya kucheza Ki-Man United. Kipa anajieleza mwenyewe, siku zote amekuwa bora,” alisema Scholes.

“Nadhani shaka ipo nani wa kucheza na Maguire. Nawapennda wengine, lakini Tuanzebe anaingia hapa.”