Samatta do or die Aston Villa

Sunday January 19 2020

Samatta do or die Aston Villa-Aston Villa- nahodha wa Taifa Stars- Mbwana Ally Samatta - Ligi Kuu England-African Lyon-Simba - TP Mazembe

 

By Thomas Ng'itu

MUDA wowote Aston Villa watamtangaza nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta a.k.a Poppa. Ni usajili ambao umeteka hisia za mamilioni ya Watanzania waliopo maeneo mbalimbali duniani pamoja na wale wa nchi jirani za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Straika huyo wa zamani wa African Lyon, Simba na TP Mazembe anatua Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England akitokea Genk ya Ubelgiji alikocheza kwa misimu minne sasa.

Safari ya Samatta kutua Aston Villa haikuka kimiujiza kwani, jitihada na umakini katika kutekeleza majukumu yake uwanjani ndio vililiweka jina lake juu ya ramani ya soka la dunia.

Hata hivyo, wakati Samatta akitimiza malengo na kiu yake ya kukipiga kwenye Ligi Kuu England, sio kuwa amemaliza kila kitu bali ndio kwanza anakwenda kukutana na changamoto mpya ambazo ni lazima azishinde ili kuthibitisha uwezo na thamani yake.

Kwa sasa Aston Villa haiku vizuri kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, iko nafasi ya 18 ikiwa na alama 21 katika michezo 22 iliyocheza kabla ya mechi yake ya jana Jumamosi dhidi ya Brighton.

Aston Villa walifuata huduma ya Samatta, ambaye ameifungukia Genk mabao 10 mpaka sasa ili kuziba pengo la straika wao Wesley atakayekuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima akiuguza majeraha ya goti.

Advertisement

Mwanaspoti limezungumza na wachambuzi wa soka nchini kuhusu changamoto mpya za Samatta wakati huu ambapo, mabosi na benchi la ufundi la Aston Villa wanamuangalia kama mtu sahihi wa kuwasaidia kuwavusha kwenye janga la kushuka daraja.

Aliyekuwa kocha wa Samatta wakati akiichezea timu ya mkoa wa Temeke, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’, alisema juhudi ndio kitu kikubwa kilichombeba Samatta kufikia mafanikio hayo.

“Samatta wakati anacheza katika timu ya mkoa wa Temeke ndio alikuwa mdogo, nakumbuka alikuwa anatoka shule na kuja kufanya mazoezi. Alikuwa na changamoto kubwa kwa sababu kulikuwa na wakubwa kama Rashid Gumbo na wenye uwezo zaidi yake, lakini hakukata tamaa kupambana na kujituma,” alisema.

Alisema anafurahia maendeleo ya Samatta kwa kuonyesha bidi na kueleza kwamba, iwe funzo kwa wachezaji wenye uwezo kutafuta nafasi ya kucheza soka la kulipwa mapema nje ya nchi ili kukimbizana na umri.

“Sina shaka kabisa na kipaji chake na ninamfahamu vizuri sana, lakini umri wake umeanza kumtupa mkono …nadhani ana miaka 28, hili liwe funzo kwa vijana wa sasa kutafuta maisha mapema,” alisema na kuongeza: Wachezaji wakienda wakiwa kwenye umri sahihi wanapata mikataba minono yenye pesa nyingi”.

Naye mchezaji wa zamani Yanga na mchambuzi makini, Ally Mayai alisema Samatta ni mfano wa wachezaji wengi kulingana na ndoto, nidhamu ya kufata maelekezo mpaka kufanikiwa.

“Samatta alikuwa anaamini kote anapopita ni njia yake ya mafanikio, lakini vijana wengi wana vipaji ila akili zao zinawaza Simba na Yanga,” alisema.

Alisema katika Ligi Kuu England licha ya kuwa Samatta anakwenda kukutana na changamoto mpya, lakini ni silaha kubwa kwake katika kufanya vizuri.

“Nafasi ya Samatta kikosi cha kwanza ipo moja kwa moja kwa sababu straika tegemeo hayupo, hivyo anatakiwa kutumia muda huo kutengeneza jina na namba ya kudumu kwa kufunga magoli,” alisema.

Naye mchezaji wa zamani Simba, Zamoyoni Mogella alisema Samatta anaweza kufanikiwa haraka kama atakuwa mtu wa kujifunza na kuelewa kwa haraka.

“Tofauti hapo ni mazingira tu na atayazoea bila shaka, lakini soka la England wanatumia nguvu nyingi na maarifa ni mara chache,” alisema.

Alisema kwa nafasi ambayo Aston Villa ipo ni fursa kwa Samatta kufanya vizuri kwa kufunga na kuiondoa kwenye janga la kushuka daraja na hapo atakuwa amejitangaza vyema.

Advertisement