Samatta: Ndoto imetimia amkumbuka mkongwe Agbonlahor

Tuesday January 21 2020

Samatta- Ndoto imetimia amkumbuka mkongwe Agbonlahor-Mtanzania Mbwana Samatta-Ligi Kuu England-mshambuliaji Gabby Agbonlahor-KRC Genk ya Ubelgiji-Aston Villa -

 

London, England. Mtanzania Mbwana Samatta amefurahi kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Aston Villa huku akikumbushia jinsi alivyokuwa akimtazama mshambuliaji Gabby Agbonlahor alipokuwa akichezea timu hiyo ya Ligi Kuu England.

Samatta amekamilisha uhamisho wake wenye thamani ya pauni 10 milioni akitokea KRC Genk ya Ubelgiji, akiwa ni Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi Kuu England.

Katika mahojiano yake ya kwanza na VillaTV, mshambuliaji mwenye miaka 27, amefurahi kuvaa jezi ya klabu hiyo.

“Ninafuraha isiyokuwa na mfano,” alisema.

“Hii ni hatua kubwa kwa maisha yangu ya soka.

“Pia kwa Watanzania wote hii ni hatua kubwa kwa soka la nchi yangu.

Advertisement

“Kila mmoja, alikuwa akisubiria kuona kwamba siku moja kuna mchezaji wa Tanzania atacheza katika Ligi Kuu England, na leo imetimia nipo hapa.

“Nimefurahi sana.”

Samatta pia alizungumzia jinsi alivyokuwa akitazama Ligi Kuu England wakati alipokuwa mdogo.

Jinsi alivykuwa alivyokuwa akimtazama Gabby, kinara wa ufungaji wa Villa katika Ligi Kuu jinsi alivyokuwa akifunga mabao yake kwa klabu hiyo.

“Tangu nilipokuwa mtoto, nilikuwa napenda kuangalia mechi za Ligi Kuu England na moja ya timu niliyokuwa nikitazama mechi zake ni Aston Villa,” aliongeza.

“Najua vitu vingi kuhusu Aston Villa, lakini moja ni wachezaji waliokuwa wakicheza hapa siku za nyuma.

“Nilikuwa napenda kumtazama Gabby Agbonlahor wakati alipokuwa akicheza hapa,” alisema Samatta.

Advertisement