Saliboko aanza kuziita Simba, Yanga kimtindo

Tuesday December 3 2019

Saliboko -aanza- kuziita -Simba-Yanga- kimtindo-mshambuliaji -Lipuli FC- Daruesh-VPL-Michezo blog-Mwanaasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

By Yohana Challe

MAMBO mazito yanayofanywa na mshambuliaji wa Lipuli FC, Darueshi Saliboko kama anaziochokoza timu kongwe za Simba na Yanga zianze kuvizia saini yake katika kuongeza nguvu ya washambuliaji kwenye safu zao za kufumania nyavu.

Simba na Yanga mpaka sasa hali sio nzuri kwenye nafasi hizo, hata Kocha Patrick Aussems (Simba) aliwahi kuongea kutokana na uhaba wa washambuliaji aliokuwa nao, unampasa kumtumia zaidi, Meddie Kagere kutokana na John Bocco kuwa Majeruhi hivyo kukosia mbadala wake kunamuumiza kichwa, japo Miraji Athuman anajitahidi kufunga.

Mitaa ya Jangwani nako wamefunga mabao sita katika michezo mitano ya Ligi Kuu ikiwa na wastani wa bao moja kila mechi, hivyo Saliboko anaweza akawa dawa ya kupunguza makali ya kufunga na kupunguza pengo walilokuwanalo katika kuifikia Simba iliyokuwa kileleni mwa VPL mpaka sasa.

SALIBOKO NI NANI?

Alizaliwa Januari 15, 1999 na alikuwa anakipenda soka tangu akiwa mdogo na baadaye akachipukia Ashanti United (sasa Pan African) ikiwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL0 msimu wa mwaka 2015/16 hapo alidumu kwa mwaka mmoja akatimkia KMC msimu wa mwaka 2017/18 na kuisaidia timu kupanda Ligi Kuu kwa sasa.

Pia kiwango chake kilimsaidia kuitwa kwenye kikosi cha timu ya vijana cha Taifa U23 na hapo ikizidi kufungua milango kwake kwa kuonana na makocha wa timu mbalimbali ambao walikuwa wakimshauri asiogope kwenda kujaribu kwenye timu za Ligi Kuu kutokana uwezo aliokuwa nao.

Advertisement

ALIVYOTUA LIPULI

Baada ya kuhakikisha KMC ikipanda Ligi Kuu chini ya Kocha, Fred Felix ‘Minziro’ ambaye alitoka kuipandisha Singida United na sasa anakinoa kikosi cha Pamba FC, mchezaji huyo alifungua milango ya kwenda Lipuli FC.

“Nilikwenda Lipuli FC kwa majaribio, wakati huo ikiwa chini ya Kocha, Suleiman Matola ambaye naye alinikubali kutokana na kipaji nilichokuwa nacho na kunipa nafasi kujiunga na Lipuli FC, kwa kweli ilikuwa furaha kubwa kwangu kuona nakwenda kutimia malengo ambayo nilikuwa nayo ya kucheza Ligi Kuu siku moja.

“Kila mtu anamalengo yake, na wachezaji ipo hivyo ukiwa na timu za ligi daraja za chini unawaza kucheza Ligi Kuu, ukifika huku mambo nayo yanabadilika unawaza kitu kingine ili mambo yazidi kunyoka,” alisema Darueshi.

MZUKA UMEPANDA

Baada ya kupiga hat trick yake ya kwanza kwenye mchezo wa maboa Lipuli FC ikiiua Singida United mabao 5-1 kwenye Uwanja wa Samora na kumfanya kuwa mchezaji wa pili kuandika hat trick msimu huu baada ya Ditram Nchimbi kufanya hivyo kwenye mchezo waliotoka sare ya mabao 3-3 mbele ya Yanga, anasema imemfanya kujiamini zaidi.

Saliboko sasa ana mabao sita sawa na mshambuliaji mwenzake, Paul Nonga ambaye alifunga mabao mawili kwenye mchezo huo na kuzidi kumpa presha, Meddie Kagere ambaye ndiye kinara wa mabao Ligi Kuu akiwa na mabao nane.

Mshambuliaji huyo alianza kufungu ukurasa wake wa mabao msimu huu wakati wakiilaza Mtibwa Sugar 3-1, kabla ya kuja kiipiga mbili Mwadui FC kwenye mchezo uliopita, na kueleza ataendeleza moto wake kama kawaida kwenye michezo inayofuata.

CHANGAMOTO ZIPO

“Hakuna mchezo ambao unakosa changamoto kwa mshambuliaji, kikubwa ni kufanya juhudi kwenye mazoezi na unapopewa nafasi ya kucheza unajitahidi na kumshawishi kocha ili kuzidi kukupa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwasababu kikosi chetu kina wachezaji wengi na wenye uwezo mkubwa, hivyo kila mchezaji anatakiwa kufanya vizuri anapopata nafasi ya kucheza,” anasema Saliboko.

Aliongeza pamoja na kuwa na lengo la kuwa na mabao mengi msimu huu, kikubwa anachokiangali ni kuhakikisha anaisaidia timu kupata matokeo mazuri katika michezo yake ya ligi na mashindano mengine watakayocheza, japo kuna changamoto wanakabiliana nazo katika kutimiza malengo wanayojiwekea ikiwa pamoja na masuala ya ukata.

Saliboko alisajiliwa na Lipuli FC dirisha dogo la msimu wa mwaka juzi sambamba na Adam Salamba baada ya kufanya vyema kwenye majaribio yake, anasema mabeki kwa sasa wanamkamia anapokuwa uwanjani na hilo linampa wakati mgumu katika kuepuka majeraha akiamini kwa kasi aliyokuwa nayo kama ataumia itampotezea malengo.

AZIITA SIMBA, YANGA

Kwa sasa mkataba wake umesalia mwaka mmoja ndani ya Wanapaluhengo hao huku akisisitiza soka ndio maisha yake na popote anaweka kambi ili mambo yazidi kuwa sawa katika maisha na kutekeleza malengo yake.

“Kwenye maisha mambo yanabadilika kila wakati, hivyo siogopi kucheza Simba wala Yanga kutokana na kuwepo kwa wachezaji wengi wenye uwezo kuliko wangu kwenye nafasi ambayo naicheza, kitu cha msingi ni kupambana na kumfanya kocha ashawishike na kile unachokifanya uwanjani na mazoezini.

“Suala la nidhamu pia linaweza likawa kipingamizi kwa mchezaji ndio maana najitahidi kuwaheshimu wenzangu kwani bila nidhamu sitaweza kupiga hatua kwenye soka wala maisha ya kawaida kwani nayo yanaendeshwa na nidhamu ya mtu.”

ANAMKUBALI BOCCO

Saliboko anasema mmoja ya wachezaji anaowakubali Bongo ni pamoja na nahodha wa Simba, John Bocco kwani amekuwa akijifunza vitu vingi kupitia kwake hasa anavyocheza, japo Kagere naye anamkubali.

“Ukimwangalia Bocco ana vitu vingi ndani ya uwanja na hata nje huwezi ukasikia mambo ya ajabu kwake, nidhamu kaiweka mbele, uwezo wake wa kujituma uwanjani katika kuipambania timu hilo limekuwa somo kwangu kila wakati ninapocheza namkubuka mchezaji huyo kwa yale anayoyafanya ndio ninayarudia nami uwanjani.

Advertisement