Sakata la Morrison, tatizo ni mfumo!

Thursday August 13 2020

 

By EZEKIEL KAMWAGA

MPAKA mchana wa jana, licha ya ahadi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilikuwa halijaamua juu ya sakata la Bernard Morrison ‘BM33’.

Lakini juzi jioni mpaka jana usiku nimemsikia aliyepata kuwa mfadhili wa Simba, Azim Dewji, akizungumza kupitia video iliyorekodiwa na kusambazwa kwenye mtandao wa WhatsApp, akimuomba Rais John Magufuli aingilie kati sakata la winnga huyo kutoka Ghana.

Azim anamtaka Rais kuingilia jambo ambalo iko taasisi kamili inayotambulika; Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambayo inalishughulikia kwa sasa. TFF ina kamati maalumu ya kushughulika na masuala ya namna hii wenye uzoefu wa kisheria na kitaasisi kushughulika na mambo haya.

Na ukimsikiliza Dewji, anashauri pia Morrison aondolewe Tanzania kwa sababu hana nidhamu na hivyo haifai Simba na pia hawezi kuaminiwa tena kuchezea Yanga kwa sababu ya alichokifanya kwenye sakata hili.

Kwa Azim na watu wengine wanaofahamika kama watu wa mpira hapa Tanzania, suluhisho la migogoro ya namna hii ni la kisiasa. Haipaswi kuwa hivi.

Jambo hili au kadhia hii ya Morrisson ni rahisi sana kwa sababu inaweza kutumika sheria na teknolojia pekee pasipo kutumia mamlaka za kisiasa. Teknolojia inaweza kutumika kujua kama kuna kughushi au hakuna na sheria inatumika kuangalia tu kwamba katika mazingira hayo, kanuni na sheria zilizopo zinasemaje.

Advertisement

Sakata la endapo mkataba wa Morrison ni halali au si halali halikupaswa kutumia mwezi mzima au siku tatu za kujadiliwa na watu wazima. Huu ni upotevu wa muda, mali na kuleta taharuki isiyo na sababu.

Katika siku tatu zilizopita, macho na masikio ya wapenzi wa soka Tanzania yaliekezwa TFF ambako suala hili la Morrison lilikuwa likishughulikiwa.

Hii si mara ya kwanza kwa TFF – kwa maana ya taasisi, kukumbwa na sakata la namna hii. Katika miaka takribani 50 ya kuwepo kwake, TFF imepitia katika migogoro tofauti kuhusu wachezaji na sasa ilitakiwa iwe imejenga uwezo wa kuitatua kwa haraka na kwa wakati.

Huko nyuma, kuliwahi kuwa na shida kwenye mikataba ya wachezaji kama Athumani Iddi, Mrisho Ngassa, Mbuyi Twite na Kelvin Yondani na yote hiyo ilitakiwa kuweka msingi wa maamuzi yatakayoweza kufanywa na TFF baadaye.

Ni bahati iliyoje sasa kwamba FIFA imeweka mfumo wa Transfer Matching System (TMS) ambao pamoja na mambo mengine, kazi yake ni kuzuia tatizo la wachezaji kusajiliwa na timu mbili tofauti katika msimu mmoja.

Kama Ligi Kuu ya Tanzania inachezwa na Morrison aliwahi kucheza Yanga msimu uliomalizika, basi jina lake litakuwepo kwenye TMS. Kama lipo lakini kuna mambo ya kughushi, masuala ya kughushi yatashulikiwa kijinai na vyombo vya dola ambavyo vina wajibu huo. Kama halipo, basi halipo na kesi inafungwa.

Kama jambo hili dogo la mchezaji mmoja linachukua siku tatu kupata suluhisho, maana yake ni moja tu; kwamba watu wameweka teknolojia, maadili na sheria pembeni na badala yake wanatumia hisia zao binafsi kujadiliana.

Ubishi wowote wa kihisia huwa hauna mshindi wala mwisho. Hakuna mwenye majibu ya kutosha kuhusu ni shabiki gani ana raha zaidi au uchungu zaidi wakati timu yake inaposhindwa au kufungwa. Jambo la hisia halina vipimo.

Na kama watu waliopewa dhamana ya kutumia sheria, maadili na teknolojia kujibu maswali magumu na wao wakaamua kuweka vyote hivyo pembeni na kutumia hisia zao binafsi, maana yake ni kwamba kuna tatizo kubwa kuliko tunavyoliona hapa nchini.

YANGA NA SIMBA

Siku chache zilizopita, nimezungumza na mmoja wa juu kabisa wa Yanga na ameniambia kwamba kuna wakati walikuwa wamefikia uamuzi wa kuachana na mchezaji huyo mwishoni mwa msimu huu. Hiyo ni baada ya mlolongo wa matukio ya kukera na kukosa uaminifu yaliyomwandamana mchezaji huyo kutoka Ghana.

Kwa maelezo yake, Yanga sasa wanaonekana kumng’ang’ania kwa sababu tu hawataki aende Simba. Walikuwa tayari aondoke kurudi alikotoka, lakini aende kuchezea Simba.

Pengine ana hoja. Lakini tuangalie upande wa pili wa shilingi.

Tuseme Yanga wakashinda hii kesi na kuambiwa Morrison ni wao, je watakuwa na imani ya kumtumia kama waliyokuwa nayo awali? Mashabiki wao watakuwa tayari kumpokea? Wachezaji wenzake Yanga watampa ushirikiano uleule walokuwa nao?

Je, kama ikitokea kwamba wameshinda na akakataa kuwachezea kwa maelezo kwamba hataki kuchezea tena Yanga, watachukua hatua gani? Kama atakuja kupewa adhabu na TFF, akimaliza na akaja kuchezea Simba baada ya adhabu yake Yanga itakuwa imepata nini?

Kama wakishinda au kesi hii kisheria, lakini baadaye uchunguzi wa kijinai ukabaini kwamba kulikuwa na makosa ya kughushi na Yanga ikanyang’anywa pointi zote ambazo Morrison alicheza msimu huu, klabu itakuwa imefaidika namna gani na sakata hili?

Nasikitika kwamba Simba nao wamejiingiza katika jambo ambalo halina faida yoyote ya maana. Tabia alizoonyesha mchezaji husika ni mbaya na anaweza kuzirudia hata akiwa na Wekundu wa Msimbazi.

Kulikuwa na sababu gani ya kujiingiza katika sakata la namna hii katika wakati ambao klabu imetoka kutwaa ubingwa wa Tanzania na FA? Usajili wa Morrison ni muhimu kiasi gani kwa klabu kiasi cha kuiingiza katika mgogoro wa namna hii?

Morrison katengeneza nafasi ngapi za mabao msimu huu? Amefunga maba mangapi msimu huu? Ujio wake katika klabu utaongeza au kupunguza kwa kiasi gani morali na ufanisi ndani ya timu?

Hakuna mchezaji mwingine Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika nzima, Ulaya au hata Brazil wanakotoka kina Fraga ambaye angeweza kusajiliwa pasipo michezo hii ya kuigiza inayoendelea sasa?

PEPO LA MABWEGE

Katika miaka ya nyuma, Waziri wa Michezo wa sasa, Dk. Harrison Mwakyembe, alipata kuandika kitabu alichokiita Pepo ya Mabwege.

Nadhani jina hilo linasadifu kwa nchi yetu na hasa sekta hii ya michezo. Mmoja wa viongozi wa Azam amenieleza wiki hii kwamba Morrison pia aliwapigia simu kuwaambia kwamba yuko tayari kuchezea klabu yao endapo itafika dau lake.

Huyu ni mchezaji ambaye haraka haraka amebaini ameingia katika taifa la watu –nakosa neno la kistaarabu kusema, wasio na maarifa kwenye matumizi ya pesa. Inavyoonekana, ameonekana kutumia udhaifu huu aliouona.

Nimepata hadithi nyingi za wachezaji wa kigeni wanaoshangazwa na namna ilivyo rahisi kupata fedha ukiwa Tanzania kuliko pengine katika ligi nyingi barani Afrika. Hapa kuna fedha za kuokota kama utajua namna ya kucheza na hisia za watu.

Tazama suala la aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Senzo Mbatha. Pasi na shaka yoyote, asingeweza kutoka Orlando Pirates kwenda Kaizer Chiefs kule kwao Afrika Kusini kwa namna alivyohamia Yanga kutoka Simba.

Lakini, muda wake mdogo alioishi Tanzania ameona kwamba kuna watu wana pesa za kuchezea na wasio na maarifa. Uamuzi wake unaonyesha kwamba ameamua kutumia udhaifu huo uliopo kujiongezea fedha.

Tutakuja kujua baadaye ni kiasi gani Yanga imeamua kumlipa ili ‘kuikomesha’ Simba. Kama kweli Yanga ilikuwa inamtafuta mtu wa aina ya Senzo kuiongoza –kwanza ingetengeneza mfumo mzuri wa kumwezesha kufanya kazi zake na ingepata mtu sahihi wa kuifanya kazi hiyo kutoka popote duniani.

Si kweli kwamba Senzo ana miujiza katika utendaji ambayo Yanga imeona imchukue ili aihamishie kwao. Wamemchukua tu kwa sababu walimwona akiwa Simba na wakataka kuiumiza Simba.

Nilichojifunza katika sakata hili la Morrison ni kwamba mfumo wetu wa soka kama tunavyouona leo umeoza na unahitaji kufumuliwa upya.

Kwa namna ulivyofumwa sasa, itatuchukua muda mrefu kufikia mafanikio tunayoyataka.

Advertisement