SIO ZENGWE: Vitendo hivi vinashusha thamani ya soka

Muktasari:

Haiwezekani mtu akaibuka asubuhi siku ya mechi akasema ana matatizo na viongozi hivyo haweze kwenda mazoezini hadi tatizo lake liishe. Haiwezekani

SIKU ile niliposhtushwa na tukio lile la ajabu la Lamine Moro kule Dodoma, kuna wengi walinishangaa. Lakini hata wao nao walishtushwa na ukatili ule aliofanyiwa Kazimoto, lakini baada ya kumwona akiomba radhi muda mfupi baadaye walitulia na kumsifu amefanya uungwana.

Niliposhangaa huyu anaomba msamaha au ametakiwa na kocha wake afanye hivyo, kulitokea maswali mengi.

“Ulitaka afanye nini ili aonekane anaomba msamaha kwa dhati?”

Mwingine alihoji “Lamine ameomba msamaha, sasa wewe unataka nini?”

Lakini niliwajibu bila kutoa povu naangalia suala hilo katika picha kubwa zaidi ya tukio moja. Nilikuwa nahisi matukio mfululizo ya utovu wa nidhamu Yanga yanaashiria kitu fulani ambacho hakionekani kwa jicho la kuangalia tukio moja. Wengi ni wale wanaotaka mambo yaende bila ya kudadisi kama hilo ni tukio moja au lina mengine yanayofanana nalo. Kama yapo, sababu ni nini.

Wakati ule nilitaja kitendo vya Bernard Morrison kugoma kwenda Shinyanga na timu. Nikasema kuna tatizo la nidhamu Yanga na pengine tatizo ni kubwa zaidi ila linajionyesha kwa hawa wachache.

Haijapita muda Morrison ameanzisha sarakasi nyingine na akatumia mtindo uleule kuimaliza. Amekosa mechi nyingine kwa mtindo uleule hadi kushtakiana na klabu TFF. Lakini amemaliza sinema yake. Yuleyule aliyeahidi Morrison angeomba msamaha na kurudi katika timu; na kocha yuleyule aliyetangulia kusema Moro ameomba radhi kwa tukio lake la ukatili; na kocha yuleyule aliyembeba Molinga kwenda naye Shinyanga baada ya kuachwa na msaidizi wake, ndiye amesema ameshamalizana na Morrison na kilichobaki ni uongozi.

Viongozi watafanya nini baada ya kocha kujiosha mikono na kumruhusu kuanza mazoezi? Watamsimamisha asiendelee na mazoezi hadi wafikie uamuzi? Hapohapo kumbuka kuna mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho inakuja. Kuna kiongozi gani atadiriki kumchukulia hatua Morrison baada ya mzozo huo wa kutengeneza ulioisha kwa suluhisho la kutengeneza?

Hili ni tatizo ambalo liko katika klabu nyingi. Ukimwachia mamlaka kocha aendeshe timu kitaalamu, anaingiza sinema; ukisema uchukue mamlaka ya kocha ya kushughulikia nidhamu, anakuponda unampangia wachezaji.

Wachezaji wakiona huo udhaifu wanajifanyia wanavyotaka bila ya kujali vitendo vyao vinaathiri vipi timu ambayo wamesaini mkataba mzuri wa kuichezea.

Mchezaji anayekosa mechi kwa sababu ya kugoma halafu tatizo likaisha wakati mechi zishapita, anafidia vipi mechi aliyokosa kwa sababu za kijinga? Anaweza kukatwa mshahara, lakini faini hiyo itafidia vipi mechi aliyokosa?

Sheria ya kazi inaeleza taratibu za kugoma, kutoa taarifa ya siku kadhaa kwa mwajiri, chama chenye wanachama wengi kuamua ni sehemu gani ziendelee na kazi wakati wa mgomo na masuala mengine mengi. Haiwezekani mtu akaibuka asubuhi siku ya mechi akasema ana matatizo na viongozi, hivyo hawezi kwenda mazoezini hadi tatizo lake liishe. Haiwezekani.

Pengine hapa ndipo Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza) inatakiwa iingilie kati na kuanza kufikiria jinsi ya kumaliza migogoro baina ya wachezaji na viongozi bila ya kuathiri mwenendo wa timu.

Wachezaji wa timu za huko walikoendelea huwa wanafanyaje wanapotaka kuushinikiza uongozi utimize matakwa yao?

Kuna sehemu ambako chama cha wanasoka huhamasisha mechi zote zichelewe kuanza kwa angalau dakika kumi kuwafahamisha wadau kuna tatizo.

Yaani mechi iliyopangwa kuanza saa 10:00 jioni ikichelewa na kuanza saa 10:15 jioni, wanaoirusha mechi hiyo moja kwa moja watahoji ni kwa nini kwa kuwa itaathiri programu nyingine. Wadhamini pia watahoji na wadau wengine wote.

Lakini mechi itachezwa na sauti ya waliogoma itasikika na mara moja hatua zitachukuliwa. Ndani ya timu pia ni lazima kuwe na utaratibu wa wachezaji kudai haki zao. Au kila mmoja akiamka na kugundua hajalipwa sign on fee, basi agome.

Wadau ni lazima waanze kujiuliza sasa nini kifanyike kuondoa vitendo kama hivyo vinavyoondoa ladha ya mpira na kushusha thamani yake.