SIMBA YAPORA BEKI BANDARINI

Muktasari:

Mwenyewe asema hajaamini kilichotokea

SIMBA inafanya mambo yake kimya kimya na juzi ikaonyesha ubabe kwa watani wao wa jadi, Yanga baada ya kufanikiwa kuidaka saini ya beki wa kati, Ibrahim Ame aliyekuwa anaichezea Coastal Union msimu uliopita.

Ame, ambaye alikuwa pacha wa Bakari Mwamnyeto na kuwatuliza mastraika tishio, amesaini mkataba wa miaka miwili juzi Jumanne.

Usajili huo sio kikumbo tu kwa Yanga bali hata Polisi Tanzania na Coastal Union ambao, inaelezwa kwamba wao ndio walikuwa wametuma tiketi ya boti kwa mchezaji huyo kutoka Zanzibar.

Picha lenyewe lilikuwa hivi: Unaambiwa vurumai iliyotokea Bandarini, Dar es Salaam haikuwa ya kawaida kwani makomando wa timu zote tatu walitinga eneo hilo na kila upande ukimsubiri beki huyo ili kwenda kumalizana naye na kumsainisha.

Lakini, baada ya beki huyo kuwasili inaelezwa kwamba, meneja wake aliyekuwa anaongozana naye tayari alishafanya mazungumzo ya kina na Polisi Tanzania kwenda kusaini mkataba wa miaka miwili huku kukiwa na kipengele cha kupewa ajira kamili.

Hata hivyo, Simba walimnyaka juu kwa juu na kumtia kwenye gari moja ya maana huku wakiwaacha watu wa Coastal na Polisi kwenye mataa, ambapo Polisi hawakukubali wakaanza kulifuatilia gari hilo hadi lilipoingia katika ofisi za klabu ya Simba zilizopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Polisi ndio walimtumia tiketi ya boti japo na Coastal Union nao walituma tiketi mdomoni, kilichotokea bandarini wakajikuta wapo wengi na mwisho wa siku Simba walimchukua na kuondoka naye kwa kuwa, msimamizi wake naye alikuwa na mazungumzo na Simba na alishajua wamepaki wapi gari yao.”

Inaelezwa kuwa mmoja wa vigogo wa Polisi Tanzania alizama ndani ya ofisi ya Simba kujua nini kimetokea na kwanini mchezaji kafanya hivyo, lakini baadaye akanywea na kusepa zake.

AME AFUNGUKA

Mwanaspoti lilimtafuta Ame ambapo mwenyewe alikiri kwamba, hakuelewa kilichotokea zaidi ya kujikuta kwenye ndinga ya Simba na baadaye kuelezwa mchakato ulivyo.

Ame alisema alikuwa na mazungumzo ya timu nyingi ikiwemo Yanga, Simba, Polisi Tanzania na Coastal Union, lakini alipofika bandarini alijikuta akiwa haelewi kwa namna alivyobebwa fasta fasta.

“Nilikuwa nakuja kusaini Coastal, lakini pia kulikuwa na mazungumzo na watu wa Yanga, Coastal na Polisi, lakini nilivyofika ilikuwa kama muvi vile maana hata mwenyewe nilikuwa sielewi kilichotokea. Lakini, nimemalizana na Simba tayari,” alisema mchezaji huyo ambaye Yanga walikuwa wanataka ili akaungane na Mwamnyeto pale nyuma.

Usajili wa beki huyu unakwenda kuongeza nguvu kwenye ukuta wa Simba, kwani katika eneo hilo ni mabeki watatu, Pascal Wawa, Kennedy Juma na Erasto Nyoni ambao wamekuwa wakicheza pamoja.

Hata hivyo, kwa sasa Simba inasuka upya safu yake ya ulinzi pamoja na kuandaa mbadala wa Wawa na Nyoni ambao kilomita za kucheza soka la ushindani kwa muda mrefu zimeanza kukata hivyo, maingizo mapya ni maandalizi.