Rooney: Nyie wapeni Liverpool ndoo yao

Tuesday March 24 2020

Rooney, Nyie wapeni Liverpool ndoo yao, Ligi Kuu ya England ,Liverpool ,Manchester United,

 

MANCHESTER, ENGLAND . MIJADALA ni mizito kuhusu kusimamishwa kwa ligi za soka katika mataifa mengi duniani, lakini ukiomba ushauri kutoka kwa gwiji wa Manchester United, Wayne Rooney, kuhusu Ligi Kuu ya England jibu atakalokupa ni moja tu. Liverpool wapewe kombe lao.

Yaani Rooney hajali kwamba Liverpool ni wapinzani wake mara mbili – moja kwa kuwa amekulia Everton ambao ni mahasimu wakubwa wa Liverpool na pili ameshapambana nao sana kiuhasama uwanjani akiitumikia Man United.

Rooney ameweka kando uhasama wote huo, akisema kwa uwazi kwamba Liverpool wanastahili kupewa kombe lao. Anataka msimu umaliziwe kuchezwa ili kuamua timu za kupanda daraja, za kushuka na za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League.

Msimu wa Ligi Kuu ya England umeingia shakani kutokana na janga la dunia la kusambaa kwa virusi vya Corona na hivyo ligi imesimamishwa hadi Mei 2.

Wakati Liverpool wanahitaji pointi sita tu kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi katika miaka 30, straika huyo wa zamani wa United na Everton anaona kwamba Majogoo wa Anfield wameipambania heshima ya ubingwa na hawapaswi kunyang’anywa kwa kuufuta msimu.

“Liverpool watatwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Wamekuwa bora kabisa. Wamefanya kazi kubwa. Wanastahili taji hili. Hebu fikiria umelisubiri kwa miaka 30 halafu mnyang’anywe kwa staili hii? Uamuzi sahihi umefanyika (wa kwamba msimu utamaliziwa),” alisema.

Advertisement

Advertisement