Ronaldo adai yupo tayari kupiga msosi na Messi

Friday August 23 2019

 

TURIN, ITALIA. MAMBO hufika mwisho. Wakati huu wakielekea uzeeni, staa wa Juventus, Cristiano Ronaldo ameanza kupunguza makali ya uhasimu wake na staa wa Barcelona, Lionel Messi. Ametoa kauli ambayo itawafurahisha waungwana wengi.

Ronaldo, 34 amesifu upinzani uliopo kati yake na nahodha huyo wa Barcelona Argentina huku akidai yupo tayari kula katika meza moja na staa huyo wa kimataifa wa Argentina ambaye awali ilidhaniwa hawapikiki chungu kimoja.

Kwa zaidi ya miaka 10 sasa mastaa hao wawili wamechuana kuwania nafasi ya nani bora zaidi katika soka ulimwenguni baina yao huku mashabiki wakigawanyika kuhusu uwezo wao binafsi pamoja na majukumu yao ya kuzibeba timu.

Mastaa hao walikuwa na upinzani mkali zaidi wakati Ronaldo alipokuwa akikipiga Real Madrid kabla ya kuondoka kutimkia Juventus katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto kwa dau la Pauni 88 milioni.

Wote wawili wamebeba mara tano kila mmoja Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia huku kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 tuzo hiyo ikibebwa na staa mwingine nje ya wao ambaye ni nyota wa kimataifa wa Croatia, Luka Modric.

Wakati tuzo hizo zimewafanya mashabiki wagawanyike zaidi kuhusu uwezo wao, na sasa Ronaldo ameibuka na kukiri wawili hao wamekuwa wakihusudiana kuhusu kazi zao huku kila mmoja akimsukuma mwenzake kuwa bora zaidi.

Advertisement

“Sina shaka kwamba Messi amenifanya niwe mchezaji bora kama ambavyo na mimi nimemfanya kuwa hivyo. Ninaposhinda mataji inamuingia akilini na ni kama mimi tu pindi yeye anaposhinda,” alisema Ronaldo.

“Kwa ukweli nashangazwa na maisha yake ya soka kutoka katika upande wake, na mwenyewe ameshaelezea jinsi alivyoudhika wakati nilipoondoka Hispania kwa sababu ulikuwa upinzani ambao alikuwa anaukubali,” alisema staa huyo.

“Ni upinzani mzuri lakini sio wa kipekee, Michael Jordan alikuwa na wapinzani katika mchezo wa kikapu, kulikuwa na upinzani wa Ayrton Senna na Alain Prost katika Formula 1. Kitu kizuri ambacho wote walikuwa nacho ni kwamba upinzani wenye msaada,” aliongeza Ronaldo.

Ronaldo ambaye mwaka 2009 alivunja rekodi ya uhamisho ya dunia wakati alipohamia Madrid kutoka Manchester United kwa dau la Pauni 85 milioni amefichua kwa kudai kwa sasa yupo tayari hata kukaa meza moja na Messi na kula naye chakula pindi wote wawili watakapostaafu soka la kulipwa.

“Nina uhusiano mzuri wa kikazi na Messi kwa sababu kwa kipindi cha miaka 15 tumekuwa tukichangia vipindi vizuri pamoja. Hatujawahi kula chakula cha jioni pamoja lakini sioni sababu gani hatuwezi kufanya hivyo siku za usoni. Sioni tatizo kabisa,” aliongeza Ronaldo.

Ronaldo na Messi wanabakia kuwa miongoni mwa mastaa waliopata mafanikio zaidi katika soka la kisasa huku wote kwa pamoja wakiwa wametwaa mataji 63 jumla yao. Wakati Ronaldo ametwaa mataji 29, Messi ana mataji 34.

Karibu kila msimu mastaa hao wamevunja rekodi ya kufunga mabao 50 kila mmoja. Ronaldo na Messi ni miongoni mwa mastaa 28 katika historia ya soka ambao wamefunga mabao zaidi ya 500. Kwa sasa Ronaldo anashika nafasi sita na Messi anashika nafasi ya saba huku kila mmoja akiwa amefunga zaidi ya mabao 690.

Upinzani wao pia umekuwa ukifananishwa na ule wa Muhammad Ali dhidi ya Joe Frazier ambao walitamba katika ulingo wa ngumi za uzito wa juu miaka ya 1970. Lakini pia ni upinzani ambao umekuwa ukifananishwa na ule wa Roger Federer na Rafael Nadal ambao wanaendelea kutamba katika mchezo wa tenisi.

Lakini pia ni upinzani ambao umekuwa ukilinganishwa na ule uliokuwa kati ya Björn Borg na John McEnroe waliotamba pia katika mchezo wa tenisi katika miaka ya 1980.

Advertisement