NYUMA YA PAZIA: Ronaldo, maskini, staa, bishoo hatimaye bilionea

Sunday June 14 2020
ronaldo pic

UMESIKIA simulizi gani mbaya kuhusu huyu mtu. Kwanza kabisa hakutakiwa kuzaliwa. Kutokana na umaskini uliokithiri kwao Madeira, mama yake, Maria Dolores Aveiro alikaribia kuitoa mimba yake ambayo ilipatikana kwa bahati mbaya. Angemtunzaje? Hakujua.

Umesikia stori gani mbaya nyingine? Kwamba utotoni alilazimika kulala chumba kimoja na ndugu zake wanne. Ni kwa sababu ya umaskini uliotopea. Nyumba ilikuwa ndogo. Kitu cha aibu zaidi ni kwamba alilazimika kulala na dada zake angali yeye ni mwanaume.

Umesikia stori gani nyingine mbaya inayomuhusu? Kwamba baba yake mzazi, Jose Dinis Aveiro alifariki kutokana na ulevi uliopindukia mwaka 2005. Ni baada ya kujihisi hathaminiwi licha ya kulitetea taifa la Ureno katika vita za Msumbiji na Ureno.

Miaka 35 baada ya kuzaliwa kwa mtu huyu, Cristiano Ronaldo Dos Santos Aveiro, licha ya kuambatana na stori mbaya, leo ni ametangazwa kuwa bilionea. Sio bilionea wa kawaida. Anakuwa mwanasoka wa kwanza katika historia ya mchezo wa soka, kutangazwa kuwa bilionea.

Inasisimua. Anakuwa mwanamichezo wa tatu baada ya Tiger Woods na Floyd Mayweather kuwa bilionea. Sahau kuhusu wacheza tenisi maarufu duniani, sahau kuhusu wanamichezo wa fani nyingine. Ronaldo anaungana na gofu na ndondi kuwa bilionea wa tatu. Anatokea katika soka.

Jarida la masuala ya utajiri la Forbes linadai Ronaldo alitengeneza kiasi cha Pauni 83 milioni mwaka jana na hivyo kufikisha kiasi cha Pauni 789 milioni katika utajiri wake na hivyo kuwa na kiasi cha dola 1 bilioni. Ukiwa na Dola 1 bilioni, wewe ni milionea.

Advertisement

Inachosha kurudia historia ya Ronaldo katika soka. Kwamba alitoka hapa, akaenda pale, akaruka hadi kule. Inachosha sana. Kama ilivyo kwa Lionel Messi, basi ndivyo ilivyo kwa Ronaldo. Historia zao ni kama mwanga. Popote upo. Hata kama kuna giza jingi, macho yakitulia utauona mwanga.

Kwanini Ronaldo amekuwa bilionea? Kwanini sio Messi? kwanini Messi atasubiri hadi mwakani ili awe bilionea? Kwanini Pele sio Bilionea? Kwanini Diego Maradona sio bilionea? Utajiuliza maswali mengi lakini Ronaldo ana majibu yake.

Hawa wengine ni wacheza soka. Ronaldo ana kipaji maridhawa kando ya Messi. Ni hatari sana. Kazi yake ya msingi ameifanya katika ubora uliotukuka. Lakini nje ya kazi yake ya soka amejipa ajira nyingine zisizoonekana katika mwili wake.

Ronaldo ni mwanamitindo na pia ni ‘muigizaji’ wa filamu za Hollywood. Hajacheza filamu hata moja lakini ukimtazama tu unaweza kumpa kazi hii. Ukimtazama tu unaweza kumpa kazi ya kuwa mwanamitindo. Yuko bize na mwili wake kwa muda mrefu sasa.

Alirekebisha meno yake, akarekebisha muonekane wake. akatengeneza staili za nywele zake. Akajiweka katika umbo kakamavu. Yote haya yanawavutia warembo. Achana na habari ya soka. Naamini katika asilimia mia ya wafuasi wa Ronaldo mitandaoni, basi asilimia 80 wanamfuatilia kwa mambo ya soka. Asilimia iliyobaki ni kwa ajili ya muonekane wake na pozi zake.

Asilimia mia ya watu ambao ni wafuasi wa Lionel Messi katika mitandao basi asilimia 97 huenda wanamfuatilia kwa sababu za kisoka. Labda asilimia tatu ndio wanaweza kuwa wanamfuatilia kwa sababu nyinginezo.

Ronaldo kajitengenezea mvuto wa kipee nje ya soka. Haishangazi kuona ni mwanadamu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao wa Instagram. Mpaka sasa ana wafuasi 223 milioni. Kama ambavyo amempita Messi kipesa basi ndivyo alivyompita kwa wafuasi. Messi ana wafuasi 154 milioni.

Licha ya hilo, kinachoweza kukushangaza ni kwamba katika mastaa kumi wa zamani au wa sasa ambao wanaulizwa nani ni zaidi kisoka kati ya Ronaldo na Messi, basi saba kati yao watamtaja Messi. Huu ndio ukweli halisi wa upande mwingine.

Ronaldo alianza kujijenga nje ya uwanja zamani. Wakati ule akiwa na Manchester United likizo zake zote zilikuwa Las Vegas Marekani au Ibiza Hispania. Na mara zote hizo alikuwa akiibuka na mrembo mpya. Na ule muonekano wake ukamfanya hata watu wa masuala la udaku wavutike naye.

Sio watu wa udaku wa soka, hapana, hadi udaku wa masuala ya muziki, filamu na mitindo walivutika naye. Na hii ni kwa sababu pia alikuwa anatoka na warembo wengi wa fani hizo. Hii ni tofauti na Lionel Messi ambaye maishani amekuwa na mwanamke mmoja tu, Antonella Rocuzzo.

Messi amekuwa akifanya mambo yake kimya kimya. Labda ana maisha mengine ambayo yangesisimua zaidi na kuleta utata kama angeyaleta hadharani lakini yeye sio mtu wa hivyo. Hulka ya wanadamu, hasa warembo ni kumpenda mtu mwenye maisha yenye utata. Mwenye kujisikia alivyo.

Ronaldo na Messi ni wanadamu tofauti katika hilo. Hata leo jaribu kutazama. Angalia jinsi Messi alivyoenda kwao baada ya corona na angalia jinsi Ronaldo alivyoenda kwao baada ya corona. Tumeonyeshwa jumba la kifahari la Ronaldo alilonunua Madeira kwa ajili ya kujificha na corona tu. Messi tulikuwa tunamuona katika shindano tu la #stayhomechallange.

Angalia jinsi ambavyo Ronaldo alirudi Turin kwa mbwembwe kubwa akiwa na familia yake katika ndege binafsi. Messi alirudi mazoezini Barcelona kimya kimya kiasi. Maisha ya kileo hayataki uwe kama Messi. Maisha haya ya mitandao wanataka uwe kama Ronaldo.

Acha awe bilionea.

Advertisement