Kilichotokea Doha makocha, viongozi wanahusika

Muktasari:

Kilichotokea kwa kina Simbu na wenzake ni pigo kwa taifa na si wao, kwani wanapofanya vizuri taifa linahamasika kutengeneza ajira kupitia michezo ya aina mbalimbali.

ASUBUHI ya juzi Jumapili habari mbaya kwa Watanzania wapenda michezo ilitawala kwa mara nyingine baada ya wawakilishi wao kwenye mbio za dunia kule Doha, Qatar, kutoka kapa huku wanariadha watatu kati ya wanne walioshiriki mwaka huu wakishindwa kumaliza kutokana na kile kinachodaiwa kuwepo kwa joto kali.

Kabla ya mashindano hayo, Mwanaspoti lilizungumza na Alphonce Simbu ambaye aliwahi kutwaa medali ya ya shaba aliyoibeba msimu uliopita London, Uingereza, wakati Geoffrey Kirui akibeba medali ya dhahabu na Tamirat Tola wa Ethiopia akitwaa medali ya fedha.

Kufeli kwa wanariadha hao kulianza mapema kutokana na kushindwa kwa uongozi wa Shirikisho la Riadha nchini (RT), kuwajibika ipasavyo sambamba na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Tumeshuhudia maandalizi ya zimamoto kwa wanamichezo kila mara na wanapofanya vibaya, lawama zinawaangukia vijana hao, lakini wanapofanya vizuri msururu wa mapokezi Uwanja wa Ndege unakuwa mkubwa kiasi kwamba hata wale waliowasapoti wakati wa kuondoka wanaonekana hawana maana tena.

Kilichotokea kwa kina Simbu na wenzake ni pigo kwa taifa na si wao, kwani wanapofanya vizuri taifa linahamasika kutengeneza ajira kupitia michezo ya aina mbalimbali.

KILICHOTUPONZA

Walioshiriki mwaka huu, alikuwa Simbu aliyemaliza nafasi ya 16 akitumia muda wa sasa 2:13:57, Agustino Sulle, Stephano Huche na Failuna Matanga ambao hawakumaliza mbio zao.

Wanawake walioshiriki walikuwa 70, lakini 30 hawakumaliza wakati wanaume walikimbia 81 na waliomaliza walikuwa wanariadha 55 kutokana na joto kali. Pamoja na Simbu kumaliza nafasi hiyo, bingwa mtetezi Geoffrey Kirui alimaliza katika nafasi ya 13 akitumia saa 2:13:54.

Tanzania imekuwa na maandalizi mengi ya mdomoni kuliko vitendo, ndio maana hata siku wanaagwa pale Arusha, nahodha wa timu (Simbu), alisema hawezi kumzungumzia mwanariadha yeyote kwa sababu kila mmoja alikuwa anajifua mwenyewe na kocha wake, hivyo hajui lolote.

Kwa kauli ile tayari Tanzania ilikuwa imefeli japo vijana walijitahidi licha ya kuangushwa na wanaowaongoza, kwa sababu hadi sasa hata mashindano ya taifa mwaka huu hayajafanyika kwa kile kinachoelezwa mdhamini ‘amekula kona’ na kila kukicha anatoa sababu zake.

KAULI ZA MAKOCHA

Suleiman Nyambui ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa RT anasema, “kwanza RT kwa sasa hawana ushirikiano, inaonyesha RT inaendeshwa na katibu, kama nasema uongo ninaomba RT ithibitishe kwa majina na tarehe kama kamati yake ya ufundi ilikaa na kuamua timu ifanyie mazoezi Arusha.

“Nilikuwa ninaona video katika mitandao, Simbu na wenzake wakifanya mazoezi barabarani. Ninaomba kocha (Andrew) Panga na Thomas (Tlanka) atuwekee aina ya mazoezi waliyokuwa wanatoa kwa wachezaji kuanzia Julai hadi Agosti wakiwa Arusha, kama kweli RT imekuwa ya jeshi la mtu mmoja, si kawaida ya Rais wa RT ( Anthony Mtaka) kutotoa salamu za kutakia mafanikio timu yetu.”

Nyambui anasema, “tangu timu ianze mazoezi ni kiongozi gani wa BMT, TOC na Serikali ameshuhudia mazoezi yao? Wakinijibu hizo hoja ndipo natoa mtazamo wangu.”

“Tumerudi nyuma sana, ile timu tuliyoijenga kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 kwa sasa haionekani na kuna hatari ya kushindwa kuwa na wawakilishi wengi mwakani kwenye Olimpiki, kwa sasa ‘qualification’ imekuwa ngumu kwa sababu wanaume wanapaswa kuwa na muda wa saa 2:11”30, mita 5,000 dakika 13:13 na 10,000 dakika 27:28, hizi timu ni ngumu kupatikana bila kuwepo kwa mazoezi ya maana.”

Alfredo Shahanga anasema, “ukiangalia hata ile timu ya miaka miwili iliyopita nani alikuwa mzuri kama siyo Emmanuel Giniki na Simbu? Tukubaliane na matokeo kwa sababu hata shirikisho lifike wakati nalo likubali kuwa lilifanya maandalizi hafifu licha ya wanariadha wengi kulalamika hali ya hewa haikuwa nzuri kwenye mbio hizo.”

MEDALI MBILI TU

Katika mashindano 17 Tanzania imebahatika kunyakua medali mbili pekee ambayo ni ile ya Simbu ambaye katika michuano iliyopita iliyofanyika London 2017 alimaliza nafasi ya tatu na kubeba medali ya shaba, alipotumia muda wa saa 2:09:51, huku Geoffrey Kirui wa Kenya akimaliza kinara kwa muda wa 2:08:27 na Tamirat Tola wa Ethiopia akiwa wa pili kwa kutumia saa 2:09:49.

Nyingine ya Christopher Isegwe ya mwaka 2005 katika mashindano yaliyofanyika Uwanja wa Helsinki, Finland wakati Jaouad Gharib wa Morocco akiibuka na medali ya dhahabu akitumia saa 2:10:10, Isengwe alimaliza nafasi ya pili akitumia saa 2:10:21 na kubeba medali ya fedha na kuandika muda bora wa msimu (season best), huku Samson Ramadhani akitumia saa 2:12:08 na kumaliza nafasi ya tano na kuweka muda wake bora (person best).

HATARINI

Mwaka ujao, wanariadha hao wanayo kazi nyingine ngumu katika mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika Tokyo, Japan kuanzia Julai 24 hadi Agosti 9, lakini hadi sasa waliofuzu ni wawili pekee ambao ni Simbu pamoja na Failuna.

Kushindwa kuwaweka kambini vijana kwa muda mrefu ndio sababu mojawapo ya Tanzania kupotea kwenye mchezo huu unaolifanya Taifa la Kenya kutamba ulimwenguni wakati walijifunza kupitia Tanzania katika miaka ya 1960-1970 ambapo kwa sasa imeachwa mbali.

Kwa sasa, Kenya wana vilabu vingi vya riadha na udhamini mkubwa, hali ambayo inawafanya kupambana kupata nafasi ya kuitwa timu ya taifa lakini suala la kufuzu mashindano kwao si tatizo, bali kuitwa kwenye vikosi vya taifa ndiko kwenye ushindani.

Tanzania tangu imeanza kumg’ang’ania Simbu imejisahau kuzalisha wanariadha wengine. Hivi kwa siku za karibuni umemuona Eliud Kipchoge wa Kenya kwenye timu ya taifa? Vipi Tamirat Tola wa Ethiopia ambaye licha ya kuwa na medali ya fedha lakini hakujumuishwa kwenye timu ya sasa, unadhani hakufuzu? Jibu siyo kweli, bali wanatoa nafasi kwa chipukizi ndio maana ushindani unaongezeka na mwaka huu Ethiopia wamebeba medali ya dhahabu na shaba kwenye marathoni.

Hatupendi kuwekeza ndio maana hata wadhamini hawana mpango na sisi kwenye michezo. Si unakumbuka msimu uliopita Ligi Kuu Bara (ya soka) ilimalizika bila kuwepo kwa mdhamini? Lakini kwenye riadha Kenya wadhamini wanaminika.

Ukicheki ofisi za Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) huwezi kufananisha na RT ambayo imepanga, na ukiwatafuta wanariadha wala hupati shida kwani kila kambi ina sifa zake. Kuna kambi za wanariadha wa mbio fupi na wale wa mbio ndefu, lakini Bongo mchanganyiko kama wali wa sherehe. Pale Kenya kuna kambi kibao kama vile Iten, Kapsait, Kaptagat anayoishi Kipchoge; Eldoret, Mosoriot, Kipseret, Kapsabet na Nandi Hills.