Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nina wasiwasi na Stars CHAN 2024

STARS Pict

Muktasari:

  • Kupewa fursa kama hiyo ni jambo la heshima kwani inaonyesha imani kubwa ambayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linalo kwa Tanzania katika kuandaa matukio makubwa kama hilo la mechi ya ufunguzi.

TANZANIA tumepata bahati kubwa ya kuandaa mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) 2024 ambazo zitaandaliwa kwa pamoja na sisi, Kenya na Uganda.

Kupewa fursa kama hiyo ni jambo la heshima kwani inaonyesha imani kubwa ambayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linalo kwa Tanzania katika kuandaa matukio makubwa kama hilo la mechi ya ufunguzi.

Na kijiwe kinakumbuka baadhi ya matukio makubwa ya kimpira ambayo Tanzania tulipewa uenyeji katika kuyafungua au kuyafunga na tukafanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu na cha nyota tano.

Mfano ni ufunguzi wa mashindano ya African Football League na mengine ni ya shule za Afrika na pia hivi karibuni tulikuwa na tukio la kufunga pazia la mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mchezo wa fainali ambao ulichezwa visiwani Zanzibar.

Hata hivyo, wakati tuna imani kwamba tutaandaa vyema ufunguzi wa CHAN 2024, wasiwasi wa kijiwe ni kwa timu yetu ya taifa ambayo itashiriki mashindano hayo kama miongoni mwa wenyeji juu ya nini itakivuna kwenye hayo mashindano.

Maandalizi ya Taifa Stars yanaonekana kuanza kwa gia ya chini sana kulinganisha na majirani zetu Uganda ambao walianza maandalizi zamani na wanaonekana wamejipanga vilivyo kwa ajili ya kufanya vyema kwenye hayo mashindano.

TFF ambayo ndio msimamizi mkuu wa timu za taifa za Tanzania, kwa sasa inakabiliwa na presha kubwa ya masuala ya Uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo ambao utafanyika Agosti 16, mwaka huu jambo ambalo linaondoa utulivu katika kuiandaa timu.

Lakini pia wachezaji wengi tegemeo wanaounda kikosi cha Taifa Stars hawajapata nafasi ya kutosha ya kupumzika baada ya kumaliza msimu mgumu na mrefu ambao ulikuwa na idadi kubwa ya mechi za ndani na kimataifa.

Tuombe Mungu tu bahati iwe upande wetu na pia wachezaji wetu wajitoe kwa zaidi ya asilimia 100 lakini tukiendelea hivi tutakuwa na wakati mgumu kwenye CHAN.