Tunalikamata taratibu soko la Waarabu

Muktasari:
- Jamaa klabu zao zina jeuri ya fedha buana na ndio maana zinaweza kupiga hodi kwa klabu nyingi hapa Afrika na zisibishiwe kwa vile zina hela na hapa kijiweni wote tunakubali kwamba mwenye nguvu mpishe na katika soka mwenye nguvu ni timu iliyo na hela.
KWA hapa Afrika, malisho bora zaidi ya kijani yapo katika klabu zinazopatikana Kaskazini mwa Afrika ambako mataifa yote yanazungumza lugha ya Kiarabu.
Jamaa klabu zao zina jeuri ya fedha buana na ndio maana zinaweza kupiga hodi kwa klabu nyingi hapa Afrika na zisibishiwe kwa vile zina hela na hapa kijiweni wote tunakubali kwamba mwenye nguvu mpishe na katika soka mwenye nguvu ni timu iliyo na hela.
Na kwa sababu timu za Kiarabu zina mzigo wa maana, zimeweka viwango vya juu vya ubora kwa wachezaji ambao zinawasajili na huwa hazichukui mtu ilimradi tu zimeongeza namba kikosini bali zinataka wachezaji wa maana.
Kwanza wao wenyewe Waarabu mpira wanaujua kuanzia kuucheza hadi kuufundisha hivyo mtu ambaye anachukuliwa na klabu zao ni ama awe na ubora wa wachezaji wao wa nyumbani au awe anawazidi kiwango.
Hapa kijiweni tukikumbuka hiyo jeuri ya fedha na kuujua mpira ya Waarabu, ndipo tunapokubaliana kwamba Tanzania tunapaswa kujivunia kwa vile kwa sasa tunaweza kuzalisha wachezaji wa daraja la juu ambao wanakonga nyoyo za Waarabu hadi klabu zao zinapigana vikumbo kuwachukua.
Ilianzia kwa Saimon Msuva alivyotoka Yanga kwenda Difaa El Jadida ya Morocco kisha akafuatiwa na kina Nickson Clement Kibabage aliyemfuata kwenye timu hiyo na tukaona mshambuliaji Shaban Chilunda na kiungo Maka Edward wakienda hukohuko Morocco katika timu ya Moghreb Tetouin.
Baadaye Luis Miquissone akaenda Al Ahly, Clatous Chama akasajiliwa na RS Berkane kama ilivyo kwa Tuisila Kisinda na baada ya msimu wa 2023/2024 kumalizika, kina Esomba Onana na Ducapel Moloko wakaelekea zao Kaskazini mwa Afrika.
Katika dirisha dogo la usajili la msimu uliomalizika, Wydad ikamnasa Seleman Mwalimu wa Fountain Gate na katika dirisha kubwa imemsajili Stephane Aziz Ki.
Na sasa tunasikia Clement Mzize yuko mbioni kujiunga na Zamalek ya Misri hii ina maana kubwa sana kwa soka la Tanzania.