Rasmi Yanga yamtangaza Kocha mpya

Muktasari:

Yanga safari hii wamezindua wiki yao ya Mwananchi Jijini Dodoma leo Agosti 22, 2020 baada ya kufanya hivyo Zanzibar mwaka jana.

Dodoma. ZILIBAKI kuwa tetesi tu awali kuhusu kocha ajaye wa Yanga, hatimaye leo Agosti 22, 2020 mabosi wa timu hiyo wamemtangaza rasmi.

Kama ambavyo Mwanaspoti lilivyokuwa gazeti la kwanza kufichua kuhusu Kocha mpya wa Yanga, ndivyo imekuwa, Cedric Kaze ndiye Kocha mpya wa Yanga.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msola ndiye aliyemtangaza rasmi Kocha Mrundi, Cedric Kaze kuionoa timu hiyo kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Msolla, ambaye ndiye mgeni rasmi wa uzinduzi wa wiki ya Mwananchi hapa inayofanyikia jijini Dodoma mwaka huu, alisema Kaze atainoa timu hiyo kufikia mafanikio wanayoyahitaji.

"Mnaouliza kuhusu Kocha, tumeshampata Cedric Kaze kutoka nchini Burundi ambaye alikuwa Canada na taratibu zinaendelea za ujio wake nchini tayari kuanza kazi ya kuinoa timu yetu" alisema Msolla.

Mbali na hilo, Msolla pia alisisitiza kuwa Kocha huyo atakuwa na wasaidizi wake aliowapendekeza mwenyewe ikiwemo Kocha wa makipa tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.