Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ile Dabi ya Kariakoo ndo leo!

LEO Pict

Muktasari:

  • Ni mchezo namba 184 ambao tarehe yake iliahirishwa mara mbili, awali ilikuwa Machi 8, 2025, kisha Juni 15, 2025, lakini baada ya majadiliano ya kina yaliyohusisha mamlaka za soka na viongozi wa Yanga na Simba, mwishowe Juni 25, 2025 ikaamuliwa kipute kipigwe kuanzia saa 11:00 jioni.

BAADA ya danadana nyingi za mchezo wa Dabi ya Kariakoo, hatimaye ile siku ndio leo Jumatano na Dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, mbivu na mbichi zitafahamika baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa na mwamuzi raia wa Misri, Amin Mohamed Amin Omar.


Ni mchezo namba 184 ambao tarehe yake iliahirishwa mara mbili, awali ilikuwa Machi 8, 2025, kisha Juni 15, 2025, lakini baada ya majadiliano ya kina yaliyohusisha mamlaka za soka na viongozi wa Yanga na Simba, mwishowe Juni 25, 2025 ikaamuliwa kipute kipigwe kuanzia saa 11:00 jioni.



MECHI YA UBINGWA

Mchezo huu ni wa ubingwa kwani Yanga inahitaji pointi moja pekee kutetea taji, huku Simba ikizihitaji tatu kuvunja utawala wa watani zao hao wa jadi.

Msimamo wa ligi unaonyesha Yanga inaongoza ikiwa na pointi 79, Simba inafuatia na pointi 78, hivyo sare tu inaibeba Yanga wakati Simba ili iwe bingwa lazima ishinde. Kazi ipo hapo.

Uhitaji mkubwa wa kushinda ilionao Simba tofauti na Yanga, unawafanya wachezaji wa wekundi hao wa Msimbazi kuingia uwanjani na deni kubwa kwa mashabiki wao baada ya kuukosa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo tangu mara ya mwisho 2020-2021 ilipobeba taji hilo.

Yanga inasaka rekodi ya kubeba mara nne mfululizo baada ya Simba nayo kufanya hivyo kuanzia 2017-2018 hadi 2020-2021 kabla ya ubabe wao kumalizwa na Yanga.

Kwa jumla, Yanga inaongoza kwa kubeba ubingwa wa ligi mara 30, Simba inafuatia kwa kuchukua mara 22.


MBINU ZA MAKOCHA

Simba chini ya Kocha Fadlu Davids, timu hiyo inacheza kwa kasi, nidhamu na uwiano mzuri kati ya ulinzi na mashambulizi. Timu hiyo inatumia mfumo wa 4-2-3-1 unaobadilika kwa haraka kuwa 4-3-3 wakati wa kushambulia, hali inayowawezesha kumiliki mpira na kushambulia kwa idadi kubwa ya wachezaji.

Katika wachezaji wanne wa ulinzi, utawakuta Shomari Kapombe upande wa kulia na kushoto Mohamed Hussein, huku katikati ni Abdulrazack Hamza na Che Fondoh Malone.

Viungo wa chini anacheza Yusuph Kagoma na Fabrice Ngoma, wakati viungo wa ushambuliaji, pembeni Kibu Denis na Elie Mpanzu, kisha Jean Charles Ahoua nyuma ya mshambuliaji na huwa anasimama kati ya Steven Mukwala na Leonel Ateba.

Mbinu hizo hazitofautiani na Miloud Hamdi wa Yanga, safu yake ya ulinzi huundwa na Israle Mwenda beki wa kulia na kushoto Chadrack Boka, mabeki wa kati wakisimama Ibrahim Bacca na Dickson Job.

Khalid Aucho na Duke Abuya wakiwa viungo wa kati katika ukabaji, kisha viungo wa juu upande wa kushambulia kushoto na kulia kuna Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya anamsaidia mshambuliaji huku pia wakati mwingine akirudi kukaba wakati mbele akisimama Clement Mzize.

Mfumo huu pindi akikosekana Prince Dube ambaye bado anauguza majeraha.


VITA YA WACHEZAJI

Mjadala wa kipa gani atakuwa na clean sheet nyingi baina ya Moussa Camara wa Simba na Djigui Diarra wa Yanga, umefungwa baada ya Camara kufikisha 19, huku Diarra akibaki nazo 16, huku ikisalia mechi moja.

Lakini sasa kuna vita nyingine ya ufungaji bora imesalia itakayoamuliwa kwenye Dabi ya Kariakoo ikiwahusu nyota watano, watatu kutoka Simba na wawili wa Yanga.

Kwa sasa Jean Charles Ahoua wa Simba anaongoza kwa mabao akifunga 16, anafuatiwa na Leonel Ateba na Steven Mukwala wanaocheza Simba wakifunga mabao 13 kila mmoja sawa na Clement Mzize na Prince Dube waliopo Yanga.

Katika nyota hao watano, Ahoua ndiye ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo akibebwa na tofauti ya mabao matatu dhidi ya wanaomfuatia.

Ukiangalia kwa rekodi ya Dabi ya Kariakoo, hakuna mchezaji aliyefunga mabao matatu ‘hat trick’ tangu afanye hivyo Abdallah Kibadeni mwaka 1977, imepita takribani miaka 48 rekodi hiyo imedumu, hivyo ili Ahoua afikiwe au azidiwe mabao, basi rekodi hiyo itavunjwa kwa maana ya kati ya Mzize, Dube, Mukwala au Ateba apige hat trick.

Pia katika uchezaji, kuna vita ya mastaa. Ulinzi wa Simba unaoongoza na mabeki wa kati, Che Malone Fondoh na Abdulrazak Hamza watakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Mzize, huku Dube akiwa na hatihati ya kucheza kutokana na majeraha ya nyama za paja yanayomsumbua.

Upande wa pili, walinzi wa kati wa Yanga, Dickson Job na Ibrahim Bacca, watakuwa na kazi ya kumzuia Mukwala au Ateba na Kocha Fadlu amekuwa na mfumo wa kumwanzisha mmoja kati yao, huku Ahoua akicheza nyuma ya mshambuliaji huyo.

Elie Mpanzu ambaye hii itakuwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Yanga, amekuwa akicheza winga zote, akienda kulia atakutana na beki wa kushoto wa Yanga, Mkongomani mwenzake Chadrack Boka, lakini akihamia kushoto kuna Israel Mwenda. Hivyohivyo kwa Kibu Denis ambaye wamekuwa wakipishana winga na Mpanzu.

Maxi Nzengeli upande wa Yanga anayecheza winga ya kulia, atakabiliana na Mohamed Hussein ambaye ni beki wa kushoto wa Simba, huku Shomari Kapombe ambaye ni beki wa kulia wa Simba, kazi yake kubwa itakuwa ni kumzuia winga wa kushoto wa Yanga ambaye Pacome Zouzoua atakuwa hapo.

Pale kati kwenye kiungo kutakuwa na ushindani mkubwa, haijwahi kuwa rahisi Aucho, Abuya na Mudathir wanapokutana na wapinzani katika harakati za kulinda mashambulizi, sasa wanakwenda kuvaana na Kagoma, Ngoma na Ahoua.

Hapo kuna viungo wabunifu wenye uwezo wa kufunga akiwemo Mudathir na Ahoua, lakini upande mwingine viungo ‘wavunja kuni’ ambao ukienda legelege si rahisi kuchukua mpira mguuni, hapa namzungumzia Kagoma, Ngoma, Aucho na Abuya.


SIMBA YASHTUA

Katika maandalizi ya mchezo huo, bila ya matarajio ya wengi Simba haikutokea kwenye mkutano na waandishi wa habari tofauti na wenzao Yanga waliofika muda uliopangwa.

Hali hiyo imefanya presha ya hatma ya mchezo huo kuanza kwani kumekuwa na utaratibu wa kikanuni kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara, timu mbili zinazokwenda kupambana zinatakiwa kuhudhuriwa mkutano na waandishi wa habari ambao makocha na manahodha huzungumza walivyojiandaa.

Jana mapema tu wenyeji Yanga walitua katika mkutano na wanahabari na Kocha Hamdi Miloud na nahodha msaidizi Dickson Job walifika saa 4:50 asubuhi.

Hamdi na Job walitangulia kufanya mkutano huo na wanahabari na kumaliza saa 5:18 asubuhi kisha wakaondoka.

Simba ilitakiwa kufuata baada ya Yanga na mkutano wao ulitakiwa kuanza saa 5:30 asubuhi lakini mpaka saa 5:43 asubuhi walikuwa hawajatokea eneo la tukio.

Baada ya Simba kushindwa kutokea, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Karim Boimanda akafunga mkutano huo akisema ratiba zingine zitaendelea.

“Tumejitahidi kuwatafuta Simba lakini wameshindwa kupatikana, kwa hiyo ratiba itabidi ziendelee, huu ulikuwa ni mkutano wa kikanuni na hili lililotokea litaamuliwa kikanuni,” alisema Boimanda.

Baada ya kutotokea katika mkutano na wanahabari, pia Simba hawakwenda kwenye kikao cha kabla ya mechi (pre-match meeting) na kwa kufanya hivyo itakumbana na adhabu ya faini ya Sh500,00 kila kosa kwa mujibu wa kanuni.


KAULI ZA MAKOCHA

Kocha wa Yanga, Hamdi alisema kikosi kipo tayari kwa mchezo huo na wako siriazi kusaka ushindi.

Hamdi alisema watawaheshimu Simba na umuhimu wa mechi hiyo inawafanya wacheze kwa nidhamu kubwa pindi wanapokwenda kushambulia.

“Sisi Yanga, tupo tayari kwa mchezo, tumekuwa kwenye maandalizi kwa muda mrefu, kulikuwa na kuahirishwa kwa ratiba ya mchezo huu lakini tuliendelea na maandalizi, tulijua kuna siku itachezwa.

“Nafahamu tunahitaji matokeo ya aina mbili kushinda na kutoa sare ili tuchukue ubingwa, hii ni mechi ya kuamua nani bingwa lakini najua hata Simba nao wana uhitaji wa matokeo ya aina moja tu kushinda ili wawe mabingwa.

“Yanga ni timu kubwa, hatuwezi kucheza mechi kama hii kwa kukaa nyuma, tutashambulia kutengeneza ushindi wetu lakini tunajua kwamba tutatakiwa kuwa makini kwenye ulinzi, tunawaheshimu Simba ni timu nzuri,” alisema Hamdi.

Hivi karibuni, Fadlu alisema wanafahamu umuhimu wa mchezo huo, hivyo wana nafasi ya kuwa mabingwa pindi wakishinda.

“Tumepoteza mataji matatu mfululizo. Lakini sasa, baada ya miezi kadhaa ya kazi ngumu, tuna nafasi ya kuwa mabingwa kwa kushinda mechi moja. Ni jambo kubwa mno,” alisema Fadlu baada ya kutoka kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, Jumapili iliyopita.