Job, Diarra watwisha mabomu Yanga

Muktasari:
- Hiyo ni kuelekea pambano la Dabi ya Kariakoo linalotarajiwa kupigwa leo Saa 11:00 jioni, ambapo ilishuhudiwa nyota hao wakitoka wenyewe wawili vyumbani, wakifuatiwa na kipa, Aboutwalib Mshery kisha dakika tano baadae ndipo wachezaji wote wakaungana nao.
NAHODHA wa Yanga, Dickson Job na kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra wametishwa mabomu ya kikosi hicho baada ya kutangulia kuingia ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wa kupasha misuli moto yaani 'Warm-Up'.
Hiyo ni kuelekea pambano la Dabi ya Kariakoo linalotarajiwa kupigwa leo Saa 11:00 jioni, ambapo ilishuhudiwa nyota hao wakitoka wenyewe wawili vyumbani, wakifuatiwa na kipa, Aboutwalib Mshery kisha dakika tano baadae ndipo wachezaji wote wakaungana nao.
Kabla ya Job na Diarra kuingia sehemu ya kuchezea, Simba ilikuwa ya kwanza kuingia kupasha misuli huku nyota wote wakijumuika pamoja tofauti na ilivyokuwa kwa wapinzani na watani zao wa jadi, Yanga.
Yanga inaingia katika pambano hili ikihitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili itwae ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya nne mfululizo.
Iko hivi, Yanga iliyocheza mechi 29 za Ligi Kuu Bara msimu huu, ina pointi 79, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 78.
Pia, Yanga inaingia katika pambano hili ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi ya duru la kwanza kwa bao 1-0, alipojifunga beki wa Simba, Kelvin Kijiri, mechi iliyopigwa Oktoba 19, 2024 uwanjani hapo.