Rashid Juma : Mussa Mgosi ameokoa kipaji changu ,siwezi kumsahau- 2

Thursday June 27 2019

 

By Thobias Sebastian na Olipa Assa

KATIKA sehemu iliyopita ya makala haya na winga kinda wa Simba, Rashid Juma tuliona jinsi kipaji chake cha mpira kilivyomletea balaa masela wakiufunga mtaa wake kisa kuwazamisha katika mechi ya ndondo na jinsi umaarufu ulivyoanza kumletea wanawake na anavyopambana kuwakwepa. Endelea katika sehemu hii ya mwisho.

Mwanaspoti: Tukio gani la furaha ambalo unalikumbuka?

Juma: Nakumbuka ilikuwa kipindi nasoma Shule ya Msingi Tandika, nilichaguliwa timu ya mkoa ambayo ilikwenda kuweka kambi Makango Sekondari, lakini nilishindwa kwenda kucheza na kujiunga na kambi kwani kipindi hicho nilikuwa mgonjwa.

Juma: Baada ya wachezaji wenzangu kwenda kambini na kufanya mazoezi ya siku tatu niliona napigiwa simu na kocha aliyekuwa na timu hiyo usiku na kuniambia natakiwa kuwapo kambini hata kama naumwa, jambo hilo lilinipa furaha sana na mpaka kesho sitalisahau.

Mwanaspoti: Kabla ya kufika Simba ulikuwa unafanya shughuli gani?

Juma: Kabla ya kuanza kucheza mpira katika soka la ushindani nakumbuka nikiwa mdogo nipo shule ya msingi asubuhi naenda kusoma na nikirudi nyumbani nachukua karanga naenda kuuza barabarani ili kupata kipato cha kujikimu na mahitaji katika maisha ya kila siku.

Advertisement

Juma: Sikuwa nafanya biashara hiyo tu, kwani kadri maisha yanavyoendelea nilijikuta nauza mihogo, matikiti, matunda na biashara nyingine za sokoni mpaka kubeba mizigo na nilikuwa nafanya hivyo kupata pesa ya kusaidia mahitaji ya familia pale nyumbani kwani hatukuwa vizuri kiuchumi.

Juma: Wakati nafanya biashara hizo za kuuza vitu tangu nikiwa nasoma shule ya msingi nilikuwa siachi kufanya mazoezi na kucheza mpira pindi ninapokuwa na nafasi. Hapo ndiyo safari yangu ya maisha ya soka ilianza mpaka kufika hapa Simba.

Si rahisi watu kufahamu mtu unafanikiwa vipi lakini binafsi nimepitia changamoto ya kutafuta pesa tangu nikiwa nasoma shule ya msingi jambo ambalo linanifanya kipindi hiki hizi riziki ambazo napata hapa Simba kuziheshimu kwani nimepitia katika maisha magumu.

Mwanaspoti: Nani alikuona mpaka kufika Simba?

Juma: Kabla ya kuhama Tandika ambako nilikuwa naishi tangu nilipozaliwa kabla ya baba yangu kujenga huku Kongowe, kuna timu nilikuwa nachezea pale na siku moja ile timu walikuwa na mechi dhidi ya Simba ‘B’ kweye Uwanja wa JK Park pale Kidongo Chekundu. Nakumbuka nilienda kuichezea timu yangu hiyo ya Tandika na baada ya mechi kumalizika kocha wa Simba ‘B’, Nicco Kiondo aliniambia nimecheza vizuri na siku ya pili yake niende Uwanja wa Kinesi, Sinza nikafanye nao mazoezi na kama nikifanya vizuri wanaweza kunisajili.

Juma: Baada ya kufanya mazoezi na Simba walinisajili katika timu yao ya vijana, ila msimu uliopita 2017-18, katika Kombe la Shirikisho (FA), Simba walianza kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Green Worriors. Wachezaji wa timu kubwa hawakuwapo wote ndiyo kocha Joseph Omog na msaidizi wake Masoud Djuma walinipendekeza nikaongeze nguvu katika mchezo huo.

Juma: Nakumbuka sikucheza mchezo ule na tulipoteza, lakini tangu hapo nilifanya mazoezi na timu ya wakubwa ambayo ilikuwa chini ya kocha Pierre Lechantre ambaye alinikubali na kunipendekeza nisajiliwe moja kwa moja kucheza timu ya wakubwa.

Juma: Safari yangu ya kucheza Simba ndiyo ilianzia hapo na mpaka sasa nacheza hapa ingawa nina malengo ya kucheza soka mbali zaidi.

Mwanaspoti: Utamkumbuka nani katika safari yako ya soka?

Juma: Katika maisha ya soka nitawakumbuka watu wengi ambao kama nikitaja mmoja mmoja hapa sitaweza kumaliza kwani kila mmoja alinifanikishia safari yangu hii kwa upande wake na mpaka leo nafanikiwa kucheza Simba. Ila sitaweza kumsahau kocha wangu Mussa Mgosi ambaye kuna muda nilikuwa nashindwa kwenda kufanya mazoezi pale Kinesi kwavile sikuwa na nauli na biashara zangu za kutafuta riziki zilikuwa haziendi vizuri, lakini alikuwa ananipatia nauli ya kwenda na kurudi nyumbani Kongowe.

Na hata siku ambayo timu kubwa walikuwa wanataka wachezaji wakaongeze nguvu kwa ajili ya mechi ya FA, sikwenda mazoezi kwa vile sikuwa na nauli, lakini Mgosi siku ya pili alinipa nauli na kuniambia natakiwa kwenda Uwanja wa Police College Kurasini kufanya mazoezi na timu kubwa.

Mwanaspoti: Baada ya miaka kumi unajiona wapi?

Juma: Baada ya miaka kumi natamani kuwepo katika orodha ya wachezaji ambao wanatumainiwa katika timu ya Taifa na kucheza soka la kulipwa kutokea nje ya Tanzania kwani nina imani klabu yangu Simba watanitengeneza na kuwa kama njia ili kufikia malengo hayo.

Mwanaspoti: Pesa nyingi ya mpira ya kwanza uliyoipata ilikuwa ni kiasi gani?

Juma: Nakumbuka pesa nyingi ya kwanza niliipata wakati timu ya vijana ya Simba inanisajili. Nilipewa Sh 200,000 ambayo sikuwahi kuishika kwa pamoja tena ikiwa imetokana na jasho langu.

Baada ya kupata ile pesa nilirudi nyumbani na kumueleza baba, kuwa nimesajiliwa na Simba na wamenipa pesa. Wakati baba anaendelea kujifikiria nilitoa pasa nikaenda kununua godoro ambalo mpaka wakati huu ninalo. Sitaweza kuisahau pesa hiyo ndiyo maana nilienda kununua kitu cha ukumbusho tena ambacho kitakaa kwa muda mrefu, lakini baada ya hapo nilifika timu kubwa nimekutana na pesa nyingine zaidi ambazo zinanisaidia kwa kweli.”

Advertisement