Pogba hauzwi

Muktasari:

Real Madrid inataka kuboresha kikosi chake na ndio maana inataka kumchukua Pogba na Christian Eriksen kwenda kukamatia sehemu ya kiungo, huku Juventus nayo ikihitaji pia huduma ya kiungo wake huyo wa zamani arudi kikosini, ambapo mpango huo umekuwa ukifanyiwa kazi na Mkurugenzi wa Michezo, Fabio Paratici.

MANCHESTER, ENGLAND. PAUL Pogba akubali tu yaishe kwamba ataendelea kubaki Manchester United kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi baada ya mabosi wa timu hiyo kudai hawawezi kukubali ofa yoyote kutoka kwenye timu yoyote ile duniani.

Mabosi wa wababe hao wa Old Trafford wamedai watagomea ofa zote si ya kutoka kwa Real Madrid wala Juventus, ambazo zimekuwa zikitajwa kwa siku za karibuni kuwa zinahitaji huduma ya kiungo huyo wa Kifaransa.

Pogba mkataba wake wa sasa kwenye kikosi cha Man United umebakiza miaka miwili na kuna kipengele kinachowaruhusu kumwongezea mwaka mmoja kiungo huyo, ambaye si kipindi kirefu sana alisema ndoto zake ni kwenda kuichezea Real Madrid, tena chini ya Kocha Zinedine Zidane.

Lakini Man United inamtazama Pogba katika macho tofauti si mwanasoka tu wa kuwapata matokeo ya ndani ya uwanja, bali kwa mambo ya nje ya uwanja ikiwamo dili za kibiashara.

Makamu Mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward alisema Pogba ni mchezaji muhimu kwenye klabu hiyo, hivyo atapambana kwa nguvu zote kuhakikisha anabaki.

Real Madrid inataka kuboresha kikosi chake na ndio maana inataka kumchukua Pogba na Christian Eriksen kwenda kukamatia sehemu ya kiungo, huku Juventus nayo ikihitaji pia huduma ya kiungo wake huyo wa zamani arudi kikosini, ambapo mpango huo umekuwa ukifanyiwa kazi na Mkurugenzi wa Michezo, Fabio Paratici.

Lakini Manchester United wala haina shida na Juventus kwa sababu inafahamu wazi haina pesa za kutosha kumsajili Pogba, kiungo huyo ambaye wao (United) ilimsajili kwa Pauni 89 milioni kwenye majira ya kiangazi ya mwaka 2016.